Siasa hizi zitawaponza, Sudi awaambia Matiang'i na Kibicho
NA OSCAR KAKAI
Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, amedai kwamba Waziri wa Usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i na katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho wamesahau majukumu yao na kuanza kujihusisha na siasa za urithi za mwaka wa 2022.
Mbunge huyo aliwasuta wawili hao kwa kujihusisha kwenye siasa na kutelekeza kazi ambayo wamepewa kikatiba.
Bw Sudi aliwasema wawili hao wanashughulika kuhakikisha ni nani atayekuwa rais 2022 badala ya kushughulikia masuala ya usalama.
Aliwataka wawili hao kukoma kuhusika na siasa na kuzingatia kuimarisha usalama wa Wakenya .
“Kwa miaka minne sasa, nimemtafuta Bw Kibicho bila mafanikio. Nimejaribu kumpigia simu na kumtumia ujumbe bila mafanikio,”alisema Bw Sudi.
Bw Sudi alisema kuwa asilimia 95 ya wakazi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wanaishi kwa amani isipokuwa asilimia tano ambao wanajihusisha na visa vya ujangili.
Akiongea jana katika shule ya upili ya Cheptulel kwenye mpaka wa Kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet kwenye msafara wa amani, mbunge huyo mzaliwa wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet alisema kuwa ni suala la kuvunja moyo kushuhudia visa vya utovu wa usalama Kaskazini mwa Bonde La Ufa.
Bw Sudi alisema kuwa umoja wa viongozi hao utachangia amani katika eneo la Bonde la Kerio .
Mbunge wa Sigor Bw Peter Lochakapong alitoa wito kwa maafisa wa usalama nchini kushirikiana na viongozi wa eneo hilo kukabiliana na utovu wa usalama katika eneo hilo.
“Matiang’i, Eugene Wamalwa, kamishina wa eneo hili na kamishina na kaunti wamefika hapa lakini hakuna lolote limefanyika,”alisema Bw Lochakapong.
Alisema kuwa msafara huo ambao ulianza siku ya Jumatatu mjini Eldoret utasaidia kuendeleza amani eneo hilo .