Simanzi watoto watatu wakiangamia kwenye mkasa wa moto wakilala
HUZUNI na simanzi zimetanda katika kijiji kimoja Kaunti ya Nyamira, baada ya watoto watatu wa familia moja kuangamia kwenye mkasa wa moto usiku wa manane wakiwa usingizini.
Kisa hicho cha Alhamisi asubuhi, Oktoba 17, 2024 kilitokea katika kijiji cha Nyangori, Wadi ya Gachuba eneobunge la Kitutu Masaba.
Kulingana na chifu wa Kitutu Mashariki Charles Okeri, watoto hao wenye umri wa miaka 12, tisa na minne walikuwa wamelala kwenye ghorofa ya kwanza ya nyumba yao ya ghorofa moja iliyojengwa kwa mbao na matofali mkasa ulipotokea.
Wazazi wa waathiriwa na ndugu mwingine walikuwa wamelala katika chumba cha chini.
“Ilikuwa mwendo wa saa saba usiku tuliposkia kuwa nyumba ya Bw Mogaito Tong’i ilikuwa imeshika moto. Tulikimbilia eneo la tukio pamoja na wakazi wengine kujaribu kuzima moto lakini tulizuiliwa na miale mikali ya moto huo uliokuwa ukienea kwa kasi. Moto huo ulipozimwa baadaye, watoto watatu wa Bw Mogaito walikuwa wamechomwa vibaya na waliangamia kufuatia majeraha waliyopata,” Bw Okeri alisema.
Msimamizi huyo wa kata hiyo aliongeza kuwa Bw Mogaito alipata majeraha na kukimbizwa katika hospitali iliyo karibu ili kupokea matibabu.
Bw Christopher Obae, ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika nyumbani kwa Mogaito kutoa usaidizi, alisema walijaribu kuwasiliana na kikosi cha zima moto cha Kaunti ya Nyamira lakini hawakupata msaada.
“Tulijaribu kutafuta usaidizi kutoka kwa wazima moto lakini hawakuwa wa msaada wowote. Tuliachwa peke yetu. Ilitubidi kutumia maji kutoka kwenye mto wa karibu ili kuuzima,” Bw Obae alilalamika.
Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Masaba Kaskazini Tobias Ombima alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.
“Tumeanzisha uchunguzi kubaini kilichosababisha moto huo. Tunatuma rambirambi kwa familia iliyoathirika,” mkuu huyo wa polisi alisema.
Miili ya marehemu ilihamishiwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Gucha, ikisubiri kufanyiwa upasuaji.