• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Simu ya video ya Rais  yachangamsha kijiji

Simu ya video ya Rais yachangamsha kijiji

Na JOHN NJOROGE

RAIS Uhuru Kenyatta alimshangaza mwanafunzi wa taasisi ya mafunzo ya elimu alipompigia simu kwa njia ya video kuzungumzia changamoto za mpango wa Kazi Mtaani.

Bi Ann Wanjiru, 20, alibahatika kupata nafasi hiyo ya kipekee kuzungumza moja kwa moja na Rais Kenyatta baada ya kutoa hotuba fupi ya shukrani kwa hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali kuu.

Bi Wanjiru, ambaye ni mwanafunzi katika chuo cha mafunzo ya ualimu, alipewa nafasi na Mshirikishi Mkuu wa eneo la Bonde la Ufa, Bw George Natembeya kutoa shukrani wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kazi Mtaani katika eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru.

Hafla hiyo, iliyofanyika Ijumaa jioni, iliongozwa na Katibu katika Wizara ya Ujenzi, Bw Charles Hinga.

“Nina furaha sana na tunakushuru kwa mpango huu. Ningetamani sana kukusemezesha (Rais) kuhusu jambo hili kupitia kwa video. Tunakuomba ikiwa unaweza kutuongeza muda zaidi kufanya kazi hii, kutoka siku 11 zilizotengwa,” akasema Bi Wanjiru kwa njia ya simu ya kawaida, huku akishangiliwa na wenzake.

Baada ya muda mfupi, Rais Kenyatta alimpigia simu Bw Hinga kwa njia ya video, huku msichana na wenzake wakijawa na furaha.

Rais alisema kuwa mpango huo ni nafasi nzuri kwa kila kijana nchini kupata nafasi kufanya kazi.Aliwaomba vijana hao kutosheka na siku 11 wanazohudumu, kwani hilo litawawezesha maelfu ya vijana kufaidika kupitia kwake.

Bi Wanjiru alimwambia Rais kwamba angetamani kukutana naye ili kumweleza mawazo kadhaa aliyo nayo.

“Sijawahi kufikiri kuwa ninaweza kupata nafasi kama hii maishani mwangu. Nina furaha sana kuzungumza na Rais, hasa kumwona kupitia video,” akasema.

Alieleza matumaini yake kuwa atakutana na Rais Kenyatta hivi karibuni.Kwa niaba ya vijana wenzake, alimshukuru Rais kwa mpango huo, akisema kuwa wengi wao walikuwa karibu kuanza kujiingiza katika maovu kama matumizi ya mihadarati na ulevi, hasa wakati huu nchi inakabiliwa na janga la virusi vya corona.

Vijana wengi ambao wamefaidika kwenye mpango huo ni wanafunzi na wasichana waliojifungua mapema.

You can share this post!

Maandamano holela hayawasaidii nyinyi vijana – Ali...

JAMVI: Kalonzo alivyomwokoa Ngilu kutoka kinywa cha mamba

adminleo