Sonko adai anachafuliwa jina kwa kukataa kutoa hongo
Na SAMWEL OWINO
GAVANA wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameipuuzilia mbali ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Umma ya mwaka wa 2017/2018 iliyotilia shaka matumizi ya Sh20 bilioni.
Aliiambia kamati ya Bunge la Seneti kwamba maafisa kutoka afisi ya Mkaguzi Mkuu waliandika ripoti hiyo baada ya kuwakataza hongo ya Sh100 milioni.
Hata hivyo, hakuthibitisha madai yake mbele ya Kamati ya Ukaguzi wa Matumizi ya Pesa za Umma (PAC), inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay, Moses Kanjwang’.
Alidai kuwa ripoti hiyo inayopaka tope utawala wake kuhusiana na matumizi ya pesa hizo, iliandikwa na watu waliokuwa na hasira kuwa alikataa kuwapa hongo.
“Ripoti hii iliandikwa baada ya dili ya maafisa kutoka afisi ya Bw Edward Ouko kuondoka kwangu mikono mitupu. Vita dhidi ya ufisadi visifanywe kwa njia ya ubaguzi… Baadhi ya sehemu za ripoti hii ziliandikwa kutokana na chuki na hasira; maafisa walitaka niwahonge, nikakataa,” akasema.
Huku baadhi ya maseneta wakiongozwa na Bw Kajwang’ wakimshauri aripoti madai yake kwa taasisi husika, wengine kama Bw Mithika Linturi (Meru) waliyataja kuwa mazito ambayo hayafai kupuuzwa.
“Madai haya ni mazito mno. Sisi kama kamati ya Bunge hatupaswi kuyafumbia macho,” akasema.
Lakini Bw Linturi alimtaka Gavana Sonko asihusishe afisi yote ya Mkaguzi wa Pesa za Umma na ufisadi, na kwamba huenda hiyo ilikuwa kazi ya afisa mmoja tu aliyekuwa akifanya hivyo kama mtu binafsi.
Mwenzake wa Narok, Bw Ledama Ole Kina, alimkaripia Bw Sonko kwa kutoa madai mazito dhidi ya maafisa wa serikali, ambao hawakuwa na nafasi ya kujitetea dhidi ya madai yake.