• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Sonko adokeza hatatetea ugavana 2022

Sonko adokeza hatatetea ugavana 2022

Na Collins Omulo

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko amedokeza kwamba huenda hatawania kuchaguliwa tena mwaka 2022 huku akiendelea kushinikizwa amteue naibu wake.

Alisema anachopanga sasa hivi ni kuacha jiji linalotoa huduma muhimu kama alivyoahidi wakati wa kampeni zake na kwamba anataka kuhakikisha amekabiliana vilivyo na wafisadi.

“Nataka nikiondoka niwe nimeacha sifa nzuri kama ambavyo Rais Uhuru Kenyatta anafanya sasa. Sitaki nichaguliwe tena kuwa gavana, lakini ninataka nikiondoka nikumbukwe kwa kuwapa huduma masikini na wakazi wote wa Nairobi. Hatutafanikiwa kutimiza haya yote tukiwa na siasa za pesa nane,” akasema Bw Sonko jijini Nairobi.

Gavana huyo amekuwa bila naibu wake tangu Bw Polycarp Igathe ajiuzulu mwezi Februari na sasa anakabiliwa na shinikizo jipya kutoka kila pembe ikiwemo Ikulu amteue naibu mpya.

Jumanne wiki jana, Rais Kenyatta alimtaka gavana huyo ajipange na kuendesha jiji inavyotakiwa, ikiwemo kujenga mitaro ya kupitisha majitaka kwa wachuuzi na wafanyabiashara katika soko la Gikomba.

 

You can share this post!

Ulinzi waimarishwa KCSE ikianza

Viongozi wakosoa kukamatwa kwa mlinzi aliyeitisha mshahara

adminleo