Sonko aendelea kuchapa kazi licha ya kufungiwa nje ya ofisi
Na BENSON MATHEKA
GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko, anaendelea kutekeleza majukumu yake kama gavana, licha ya kupigwa marufuku kukanyaga ofisi yake kufuatia kesi ya ufisadi inayomkabili.
Imefichuka kuwa Bw Sonko amekuwa akitumia ofisi yake ya kibinafsi katika eneo la Upperhill jijini Nairobi kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kupokea jumbe kutoka nchi za kigeni.
Mnamo Jumatatu, Bw Sonko alikutana na ujumbe wa wataalamu wa matibabu ya moyo kutoka ng’ambo katika ofisi hizo, na akatangaza kuwa walijadili ushirikiano unaolenga kuanzisha kliniki za kutibu matatizo ya moyo katika hospitali moja ya umma kaunti ya Nairobi.
“Mapema leo, ujumbe wa wataalamu wa maradhi ya moyo kutoka Amerika ulipokelewa katika ofisi zangu za kibinafsi Upperhill ambapo tulifanya mazungumzo yanayonuiwa kuanza ushirikiano wa kuanzisha kliniki ya matibabu ya moyo na kituo cha mafunzo katika moja ya hospitali zetu za umma,” Bw Sonko alisema kwenye ujumbe wa Twitter.
Aliambatisha ujumbe huo na picha nne akiwa na raia watatu wa kigeni wakifanya mazungumzo katika ofisi iliyopambwa kwa fanicha za dhahabu. Kuna bendera ya Kenya na ya serikali ya jiji la Nairobi nyuma ya kiti chake ishara kwamba alikuwa akiongoza mkutano rasmi.
Mnamo Februari 19, Bw Sonko alifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri ambapo aliwafuta mawaziri wawili na kuwarejesha kazini aliokuwa amesimamisha kazi. Aliwafuta Paul Kahiga aliyekuwa akisimamia wizara ya fedha na Winfred Gathangu aliyekuwa akisimamia wizara ya Kilimo.
Katika mabadiliko hayo alimteua Karen Nyamu kuwa waziri wa Kilimo na akamrejesha Charles Kerich katika wizara ya Ardhi.
Alichukua hatua hiyo baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji alilotaka ifute dhamana ya Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal , kwa kubadilisha baraza lake la mawaziri.
Kabla ya mabadiliko hayo, Bw Sonko alikuwa amemteua Anne Mwenda kuwa naibu gavana, hatua ambayo ofisi ya Bw Haji ilipinga ikisema alikuwa akikaidi masharti ya dhamana yake.
Kupitia wakili wake Cecil Miller, Sonko alimweleza Bw Haji kwamba hakukaidi masharti ya dhamana kwa kumteua Bi Mwenda akisisitiza kwamba angali gavana wa kaunti ya Nairobi.