Sonko aendelea kunyolewa bila maji
Na COLLINS OMULO
GAVANA wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko anaendelea kuvuliwa mamlaka zaidi baada ya Bunge la Kaunti ya Nairobi kuhamisha usimamizi wa miradi katika wadi kutoka ofisi yake hadi Idara ya Huduma za jiji la Nairobi (NMS).
Hii baada ya madiwani kuidhinisha Sh1.3 bilioni za hazina ya maendeleo katika wadi (WDF) zihamishiwe NMS.
Hatua hii inamaanisha kwamba hazina hiyo itakuwa chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa NMS Meja Jenerali Mohammed Badi na wala sio serikali ya Sonko.
NMS sasa itasimamia miradi ya maendeleo katika wadi 85 za Kaunti ya Nairobi na kutia nguvu idara hiyo katika usimamizi wa huduma katika serikali ya kaunti hiyo huku Gavana Sonko akivuliwa mamlaka kabisa.
Madiwani walimpokonya jukumu hilo saa chache baada ya kutengea NMS Sh27.1 bilioni katika bajeti ya mwaka wa kifedha utakaokamilika Juni 30 2021 huku wakitengea serikali ya kaunti Sh6.4 bilioni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Katika Bunge la Kaunti ya Nairobi Robert Mbatia alisema kwamba hazina hiyo sasa itakuwa chini ya NMS.
Alieleza kwamba hazina hiyo haingeendelea kusimamiwa na Gavana Sonko kwa sababu wahandisi wote wanaofaa kusimamia miradi sasa wako chini ya NMS kwa kuwa huduma za ujenzi ni jukumu lililohamishwa kwa serikali ya kitaifa.
“Sijawahi kufahamu kwa nini hazina hiyo iliwekwa katika ofisi ya gavana kwa sababu awali, ilikuwa kamati ndogo ya kamati ya ujenzi. Hili ni jukumu ambalo tulipeleka inapofaa kuwa,” alisema Bw Mbatia.
Kwenye bajeti ya kaunti ya mwaka wa kifedha utakaokamilika Juni 30 2021 iliyopitishwa Alhamisi, hazina ya maendeleo katika wadi ilitengewa Sh1.3 bilioni huku Sh30 milioni zaidi zikitengwa kulipa mishahara.
Hatua hii ni baraka kwa madiwani wa kaunti ya Nairobi ambao wamekuwa wakilaumu serikali ya Gavana Sonko kwa kuwanyima pesa za kufadhili miradi ya maendeleo katika wadi zao.
Mwaka jana mwenyekiti wa kamati ya WDF, Patricia Mutheu alilalamika kwamba serikali ya kaunti haikuwa imetekeleza hazina hiyo tangu sheria ya kuibuni ilipopitishwa 2014, ikisingizia vikwazo vya mdhibiti wa bajeti.
Alilaumu gavana kwa kushindwa kutekeleza miradi yoyote yenye maana licha ya kutengewa pesa na kushirikishwa katika mpango wa maendeleo wa kaunti.
Bi Mutheu ambaye ni diwani wa wadi ya Mlango Kubwa alisema miradi ambayo ilianzishwa na serikali ya Sonko ilikwama.