Habari MsetoSiasa

Sonko akanusha mipango ya kujiuzulu kwa kulemewa na kazi ya ugavana

March 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na WYCLIFFE MUIA

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko Jumatano alikanusha taarifa kuwa anapanga kujiuzulu kutokana na changamoto anazokumbana nazo katika uongozi wake.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Sonko alikashifu vyombo vya habari kwa kueneza propaganda kuwa anapanga kujiuzulu kama gavana wa Nairobi.

Habari zilizodaiwa kuchapishwa katika mtandao wake wa Facebook zilisambaa zikisema gavana huyo anaendelea kusaka ushauri kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu.

“Mjue hii kazi imekuwa ngumu (na) iko karibu kunishinda. Na sio mambo ya bendera. Hizo nimekubali kutoa kama nilivyoshauriwa na (Katibu wa Usalama wa Ndani) Karanja Kibicho lakini nitawaambia hivi karibuni ni kwa nini nataka kung’atuka mnishauri. Isiwe kama yule ndugu yangu alihepa bila kusaka ushauri,” taarifa iliyodaiwa kuchapishwa katika Facebook yake ilinukuu.

Inaaminika usemi wa ‘ndugu yangu aliyehepa bila kusaka ushauri’ Sonko ulirejelea naibu wake Polycarp Igathe ambaye alijiuzulu mnamo Januari 13, kwa misingi kuwa hangeweza kuaminiwa na gavana huyo.

Hata hivyo, kupitia akaunti yake ya Twitter Jumatano, Sonko alisema yeye anajishughulisha na uchapa kazi na wala hana nia ya kuacha kazi ya ugavana.

“Wacheni propaganda ya pesa nane ati nataka kujiuzulu. Uzeni stori zenu wachaneni na mimi nifanye kazi,”aliandika Sonko.

Mapema wiki hii baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya, walimshtumu Sonko, kwa kudai kwamba wanasiasa wa eneo hilo wanapanga kuhujumu azma ya Naibu Rais William Ruto ya kutwaa urais 2022.