Habari Mseto

Sonko amejihami vilivyo kuokoa kazi yake isimtoke

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi, Bw Mike Sonko, anajiandaa kukabili madai yaliyotolewa dhidi yake na madiwani ambao walimtimua mamlakani wiki iliyopita.

Msemaji wa Bw Sonko, Bw Ben Mulwa, alisema kuwa gavana huyo ana mawakili watakaomsaidia kuendesha kesi yake mbele ya Seneti kwa kuwasilisha ushahidi, huku pia akieleza uwezekano wa kuelekea mahakamani kupinga kung’atuliwa mamlakani.

“Tayari Gavana ameanza kukutana na mawakili wake ili kuandaa ushahidi ambao atawasilisha kwenye Seneti. Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa hatuna nia ya kwenda mahakamani. Atahitaji kujiandaa kujitetea Seneti ama mahakamani,” akasema Bw Mulwa.

Kambi ya Bw Sonko inadai uwepo wa njama kuhusu namna hoja ya kumng’oa mamlakani ilivyoendeshwa.

Diwani Mwangi Njihia wa wadi ya Woodley/Kenyatta Golf Course, alisema ushahidi wao utakuwa wenye uzito.

“Tutamwendea Spika sasa. Lazima waieleze mahakama na Seneti jinsi walivyopata madiwani 88 ilhali tuko 57. Tuko pamoja na gavana tukimsaidia kuandaa mikakati ya kujitetea,” akasema Bw Njihia.

Bw Sonko alijikuta pabaya baada ya hoja hiyo kufaulu, licha ya kuwasafirisha madiwani 57 nyumbani kwake katika Kaunti ya Kwale.

Hoja hiyo iliwasilishwa na Kiongozi wa Wachache kwenye Bunge la Kaunti, Bw Michael Ogada.

Bw Ogada, ambaye ndiye diwani wa Embakasi, alisema Bw Sonko alifanya kosa kubwa.

“Kosa kubwa alilofanya ni kuwapa madiwani simu kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa. Tulitumiwa namba zao mpya za simu baada ya muda mfupi tu. Baadaye, tuliwatumia mfumo ambao wangeweza kupiga kura kupitia Zoom. Ni hali iliyompata Bw Sonko na washirika wake kwa mshangao. Iwapo hangetaka wapige kura, hangewapa namba mpya za simu,” akasema.

Bw Ogada, ambaye alichaguliwa kwa chama cha ODM, alisema tayari chama hiccho kilikuwa kishatoa msimamo wake, hivyo hangebadilisha mpango wowote kuhusu suala hilo.

“Watu wengi walitumwa kwangu wakiwa na pesa kujaribu kunishawishi kubadilisha msimamo wangu. Mara ya kwanza, waliahidi kunipa Sh5 milioni. Baadaye, waliongeza kiwango hicho kuwa Sh15 milioni. Hawakufa moyo, kwani walifikisha kiasi hicho kuwa Sh30 milioni. Hata hivyo, nilikataa rai zao na kuwafukuza,” akasema.

Kwa kuhofia angeshindwa, Bw Sonko alianza kudai kuwa akaunti za baadhi ya madiwani aliokuwa nao “zilidukuliwa na kuingiliwa” bila ufahamu wao.

Baada ya patashika hiyo, aling’olewa mamlakani kama gavana baada ya zaidi ya madiwani 80 kupiga kura kuunga mkono hoja hiyo. Ni madiwani wawili pekee waliopinga.

Cha kushangaza ni kuwa karibu madiwani 30 kati ya 57 waliokuwa pamoja na Bw Sonko ni miongoni mwa 86 waliokuwa wametia saini zao kuunga mkono hoja hiyo wiki iliyopita.

Akitangaza matokeo ya hoja hiyo, Spika Benson Mutura alisema madiwani 88 walipiga kura kuunga gavana kung’olewa mamlakani.

Idadi hiyo iliongezeka kwa madiwani wawili zaidi, kwani ni 86 kati yao waliokuwa wametia saini kuunga mkono hoja hiyo. Licha ya kukisiwa kuwarai zaidi ya madiwani 90 kupinga hoja hiyo, ni madiwani wawili pekee waliomuunga mkono.