Sonko ampa kazi dadake Raila
Na CHARLES WASONGA
GAVANA wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko amemteua dadake kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa wadhifa katika serikali ya kaunti hiyo.
Bi Beryl Odinga ameteuliwa kuwa mwanachama wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Maji ya Nairobi (Nairobi Water Company).
Akiongea na wanahabari Jumatano Mkurugenzi wa Mawasiliano katika afisi ya Gavana Sonko Bw Jacob Elkana alisema kuwa kigezo kilichozingatiwa katika uteuzi huo ni uwezo mteule kutoa huduma kwa umma.
“Naweza kuwa dadake Raila au mtu kutoka ukoo wake. Lakini Nairobi sio mali ya Sonko, ni ya wakazi wote wa kaunti hii. Kwa hivyo mtu yeyote aliyehitimu anaweza kupewa nafasi ya kuwahudumia wakazi katika wadhifa wowote ule,” akasema.
Bw Elkana akaongeza: “Uteuzi huu haujafanywa kwa misingi ya siasa, hauhusu kabila bali unahusu huduma utakaotolewa kwa wakazi wa Nairobi.
Bodi mpya ya wakurugenzi wa kampuni ya Nairobi Water iliteuliwa Jumatano na itaongozwa na Bw Paul Kardos kama mwenyekiti.
Wanachama wengine wa bodi hiyo ni; aliyekuwa Waziri wa ICT katika kaunti ya Nairobi Emma Mukuhi, aliyekuwa mhariri wa Capital FM Michael Muma, Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Nairobi Timothy Muriuki, Mohammed Abdulahi, Martin Mbicire, Charles Kerich, kaimu katibu wa kaunti Leboo Morintat na aliyewania wadhifa wa mwakilishi wa wanawake Nairobi Bi Karen Nyamu.