Sonko apinga kufufuliwa kwa kesi dhidi yake
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA Gedion Mike Sonko Mbuvi Jumanne aliomba Mahakama ya Rufaa isiruhusu kufufuliwa kwa kesi ya kupinga ushindi wake na walalamishi wawili walioshindwa kuendeleza kesi hiyo katika Mahakama Kuu.
Mawakili Cecil Miller na Harrison Kinyanjui waliwaambia majaji Roselyn Nambuye , Gatembu Kairu na Kathurima M’Inoti kwamba Mabw Japheth Muroko na Zacheaus Okoth walipewa fursa ya kuwasilisha ushahidi dhidi ya Sonko lakini wakakwepa.
“Haiwezi kuchukuliwa kama mzaha kwamba maelfu na maelfu ya wafuasi wa Sonko walikuwa wanatarajia kuona ushahidi ambao ungeliwasilishwa na walalamishi hao. Matarajio yao yaliambulia patupu,” alisema Kinyanjui.
Kinyanjui alisema walalamishi hao wawili hawakuwasilisha ushahidi kwamba walitishwa kiasi kwamba hawangefika kortini.
Muroko aliambia korti kupitia kwa wakili Antony Oluoch kwamba alipokea vitisho na kuripoti katika kituo cha polisi cha Kilimani.
Kinyanjui alisema Dkt Akala alikuwa mmoja wa mashahidi.
Wakili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, Nani Mungai aliunga mkono ushahidi wa Sonko na kuomba korti isikubali kufufuliwa kwa kesi hiyo.
Mahakama itatoa uamuzi Aprili 13.