Habari Mseto

Sonko baridi Babayao akizama

January 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

LEONARD ONYANGO na MAUREEN KAKAH

GAVANA Mike Sonko wa Nairobi ameingiwa na baridi baada ya jirani yake Ferdinand Waititu kunyolewa ugavana na maseneta mnamo Jumatano.

Bw Sonko anakabiliwa na masaibu sawa na Bw Waititu na hatua ya Seneti pamoja na bunge la Kaunti ya Kiambu kupitisha hoja ya kung’oa gavana huyo ina uwezekano mkubwa wa kujirudia Nairobi.

Magavana hao wawili wameshtakiwa kwa madai ya wizi wa mamilioni ya pesa za umma na pia wamekatazwa kufanya kazi zao za kaunti hadi kesi dhidi yao zisikizwe na kuamuliwa.

Sawa na Kiambu ambapo madiwani waliungana na kupiga kura ya kumwondoa Bw Waititu, katika Kaunti ya Nairobi pia kumekuwa na juhudi za kuwasilisha hoja sawa na hiyo dhidi ya Bw Sonko.

Bunge la Nairobi linatarajiwa kurejelea shughuli zake Jumanne ya Februari 11 baada ya likizo, na huenda hoja ya kutaka kumtimua Gavana Sonko ikaibuliwa tena.

Awali, madiwani wakiongozwa na Spika Beatrice Elachi walikuwa wametangaza mpango wa kumtimua Bw Sonko lakini hoja hiyo ikafifia baada ya mgawanyiko kuibuka miongoni mwa madiwani.

Kumekuwepo na madai ya visa vya hongo katika harakati za kuzuia madiwani kujadili hoja ya kumtimua Sonko.

Wakili Steve Ogola anasema kuwa kutimuliwa kwa Gavana Waititu kunafaa kumtia wasiwasi Gavana Sonko: “Gavana Sonko anakabiliwa na mashtaka sawa na yaliyomfanya Bw Waititu kutimuliwa. Madiwani wakiamua kumtimua itakuwa vigumu kwake kunusurika katika Seneti.”

Bw Sonko sawa na Bw Waititu pia anaonekana kukosa uungwaji mkono wa serikali kuu, ambapo mara kadha amelalamika kuingiliwa kikazi na maafisa wakuu serikalini.

Katika juhudi za kumwondoa Bw Waititu, mkono wa serikali kuu ulionekana katika shughuli hiyo huku mrengo unaoegemea handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ukishikana kupiga kura ya kumng’oa Bw Waititu.

Sawa na Kiambu, huduma jijini Nairobi zimetatizika tangu Bw Sonko alipozimwa na korti kuingia ofisini, suala ambalo lilitumiwa na madiwani wa Kiambu kusukuma ajenda ya kumwondoa Bw Waititu, jambo ambalo linaweza kujirudia Nairobi.

Jana, Gavana Sonko alidai kuwa baadhi ya maafisa katika serikali ya Kaunti ya Nairobi wanamhujumu kwa kukataa kuzoa takataka ambazo zimetapakaa kila kona jijini.

Ni masuala haya ambayo yamemweka baridi Gavana Sonko akihofia wembe uliomnyoa mwenzake wa Kiambu huenda ukatiwa makali tena dhidi yake.

Gavana wa Samburu

Kutimuliwa kwa Bw Waititu pia kumemtia hofu Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal ambaye pia alizuiliwa kwenda afisini baada ya kufikishwa kortini na kushtakiwa kwa madai ya kuhusika na ufujaji wa fedha za umma.

Watatu hao walipigwa breki kuendesha shughuli za kaunti kufuatia uamuzi uliotolewa na Jaji Mumbi Ngugi aliyesema kuwa wakuu wa kaunti wanaokabiliwa na kesi za ufisadi wasiruhusiwe kutekeleza majukumu yao.

Katika uamuzi wake, Jaji Ngugi alishikilia kuwa magavana sawa na watumishi wengine wa umma wanafaa kujiondoa kwa muda wanapofikishwa kortini kujibu mashtaka ya ufisadi, na shughuli za kaunti ziendeshwe na manaibu wao.

Mahakama Kuu mnamo Desemba ilikataa ombi la kutaka madiwani wazuiwe kumtimua Gavana Sonko.

Hapo jana Bw Waititu alienda mahakamani kupinga uamuzi wa Seneti kumwondoa madarakani.

Jaji wa Mahakama Kuu James Makau aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuipanga kusikizwa Jumatatu ijayo.

Bw Waititu pia anataka shughuli ya kuapishwa kwa naibu wake James Nyoro kusitishwa.