Sonko ni kufa kupona akijaribu kujinusuru leo
Na COLLINS OMULO
SENETI leo Jumatano itaandaa kikao spesheli kuanza kusikiliza kutimuliwa kwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko.
Kikao hicho kilitarajiwa kufanyika Alhamisi na Ijumaa lakini sasa kitaanza leo na kukamilika Alhamisi baada ya spika wa seneti, Bw Kenneth Lusaka kukisongesha mbele kwa siku moja.
Kupitia ilani katika gazeti rasmi la serikali, Bw Lusaka alisema kwamba uchunguzi kuhusu mipango ya kumuondoa Gavana Sonko ofisini utaanza saa tatu asubuhi katika seneti, kwenye majengo ya bunge.
Uchunguzi huo unafuatia kikao cha seneti wiki jana ambapo iliamuliwa Gavana Sonko atahojiwa na kikao cha maseneta wote baada ya madiwani kupitisha aondolewe ofisini.
“Kulingana na sehemu ya kwanza ya kanuni nambari 30 ya seneti kuhusu ombi la Kiongozi wa Wengi katika seneti na kwa kuungwa mkono na idadi ya maseneta inayohitajika, nimeteua Jumatano Desemba 16, 2020 na Alhamisi Desemba 17, 2020 kuwa siku za kikao spesheli cha seneti kuchunguza pendekezo la kumuondoa ofisini Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko,” alisema Bw Lusaka.
Alisema kwamba katika siku hizo mbili, vikao vitakuwa vikianza saa tatu asubuhi kujadili pendekezo la kuondolewa kwa Sonko pekee kabla ya seneti kuahirisha shughuli zake hadi Februari 9, 2021.
Bw Sonko anakabiliwa na mashtaka kadhaa mbele ya seneti yakiwemo ukiukaji wa katiba na sheria nyingine, matumizi mabaya ya ofisi, kutenda uhalifu chini ya sheria na kutokuwa na uwezo wa kiakili kusimamia serikali ya kaunti.
Kwenye kikao cha leo, maseneta watapatiwa muda wa kutoa rambirambi zao kufuatia kifo cha mwenzao wa Machakos Boniface Mutinda Kabaka kabla ya kuzamia ajenda kuu ya kumchunguza Bw Sonko.
Kutakuwa na kikao cha faragha ambapo maseneta watafafanuliwa na mawakili wao kuhusu mashtaka dhidi ya Sonko na ushahidi uliowasilishwa kabla ya kuanza kikao cha wazi kuanzia saa tano mchana.
Bw Sonko atasomewa mashtaka yote manne yaliyoongozwa na Kiongozi wa Wachache katika bunge la Kaunti, Bw Michael Ogada kabla ya maseneta kupumzika kwa chakula cha mchana.
Baada ya chakula hicho, pande zote zitatoa taarifa za mwanzo. Bunge la Kaunti ya Nairobi litapewa saa nne kueleza mashtaka dhidi ya Sonko wakiongozwa na wakili Ndegwa Njiru.
Katika muda huo, watawasilisha ushahidi na mashahidi na kuhojiwa na mawakili wa Sonko.
Katika kikao cha Alhamisi, Bw Sonko na mawakili wake watapewa saa nne pia kujibu mashtak dhidi yake na kuwasilisha mashahidi ambao wataulizwa maswali na mawakili wa bunge la kaunti.
Baadaye kila upande utapewa muda wa kuwasilisha taarifa ya mwisho kabla ya maseneta kufanya kikao cha faragha kujadili mawasilisho kabla ya kurudi kwa kikao cha wazi kupiga kura.
Huwa kuna maseneta 47 waliochaguliwa lakini kwa sasa ni 46 kufuatia kifo cha Seneta Kabaka watakaopiga kura kuamua hatima ya Bw Sonko.