• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Sossion awataka wazazi wawe watulivu majadiliano kuhusu elimu yakiendelea

Sossion awataka wazazi wawe watulivu majadiliano kuhusu elimu yakiendelea

Na CHARLES WASONGA

KATIBA Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion amewataka wazazi kudumisha utulivu huku wizara za Afya na Elimu zikishauriana kuhusu uwezekano wa kufunguliwa tena kwa shule.

Kwenye mahojiano ya asubuhi katika runinga ya Citizen, Jumatano, Novemba 4, 2020, Bw Sossion pia ameunga msimamo wa Waziri wa Elimu George Magoha kwamba wanafunzi wa Gredi ya Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne wasalie shuleni.

Hii ni licha ya ongezeko la visa vya maambukizi ya corona shuleni tangu zifunguliwe mnamo Oktoba 5, 2020, ambapo walimu wawili wamefariki.

“Nawaomba wazazi na wadau wengine kuwa watulivu wakati huu ambapo visa maambukizi ya corona vimeongezeka hata katika baadhi ya shule. Najua kwamba maafisa wa wizara za Elimu na Afya wanajadiliana kwa lengo la kuruhusu wanafunzi wa madarasa mengine warejelee masomo,” akasema.

Kauli ya Bw Sossion imejiri saa chache baada ya watahiniwa 52 wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kolanya iliyoko Busia kupata virusi vya corona.

“Ukisema kuwa wanafunzi wa Shule ya Kolanya wanafaa kuenda nyumbani, utakuwa ni kama unasababisha kuenea kwa virusi vya corona katika ngazi ya kijamii,” akasema Katibu huyo Mkuu wa Knut ambaye pia ni mbunge maalum.

Bw Sossion amesema wanafunzi wako salama katika shule kuliko walivyo kule nyumbani, akiongeza kuwa shule zifunguliwe kikamilifu.

“Kile ambacho tunapaswa kujadili wakati huu ni namna ya kufungua shule kwa utaratibu ambao hautahatarisha maisha ya wanafunzi kutokana na ugonjwa wa Covid-19,” akaeleza.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Tumia ubora ulio nao kufanyia kazi bora...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo muhimu katika...