Sportpesa yafichua imekuwa ikipata faida ya Sh54 milioni kila siku
Na PETER MBURU
KAMPUNI ya michezo na Kamari Sportpesa 2018 ilikuwa ikipata faida ya Sh38, 051.75 kila dakika, ama Sh634 kila sekunde kutoka kwa watu waliotumia pesa zao kubashiri michezo.
Kiwango hicho ni sawa na kusema Sportpesa kila saa ilikuwa ikipata Sh2.28 milioni, ama Sh54.8 milioni kila siku.
Hesabu hizi ni kutokana na chapisho la kampuni hiyo katika gazeti la Standard Jumatatu kuonyesha jinsi iliingiza na kutumia pesa mwaka 2018, ambapo ilisema kuwa ilipata Sh20 bilioni.
Sportpesa katika tangazo hilo ilisema kutokana na pesa hizo ilipata faida ya Sh9 bilioni kwa jumla, na ikalipa ushuru wa Sh6.4 bilioni.
Vilevile, kampuni hiyo ilisema ilitumia kiwango kikubwa cha pesa kusaidia jamii, hasa kuinua michezo, elimu na kilimo.
Sportpesa ilisema ilitumia Sh693 milioni kufadhili michezo ya kandanda, Sh600 milioni kufadhili michezo ya raga, Sh75 milioni kufadhili michezo ya ubondia, Sh73 milioni kufadhili kilimo, Sh57 milioni kufadhili elimu na miundomsingi na Sh41 milioni kufadhili afya ya jamii.
Matumizi haya, kulingana na kampuni hiyo, ni licha ya ufadhili ambao ilitoa kwa michezo, mashirika na timu zingine, kama AFC Leopards, FKF, Sportspesa Shield na kwa mwanabondia Fatuma Zarika.