Habari Mseto

Stovu za kawi safi zazinduliwa Nakuru

June 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

RICHARD MAOSI na MAGGY MAINA

KWA jumla, takriban watu bilioni 1.5 kote ulimwenguni wanaishi bila umeme kutokana na ukosefu wa miundomsingi na pia gharama ya juu ya stima.

Kupitia uchunguzi uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO ), watu milioni nne hupoteza maisha yao kila mwaka kutokana na maradhi ya kupumua yanayosababishwa na kawi chafu.

Hali hii kachangiwa na kawi ambayo sio safi kama vile mafuta taa na makaa ambayo hupatikana mitaani kwa bei nafuu.

Tabia ya binadamu kutegemea nishati ya kawi kutokana na miti, imechangia uharibifu wa mazingira na kuchochea ukame katika baadhi ya maeneo.

Ikumbukwe kuwa miti ndiyo huvuta mvua na mara nyingi kuzuia mmomonyoko wa udongo .

Ni kwa sababu hiyo National Council of Community Based Organisation (NCCBO) kwa ushirikiano na kampuni ya Toyokomi kutoka Japan, wamebuni stovu aina ya kipekee itakayosaidia kutunza mazingira.

Mradi wenyewe unalenga kunufaisha familia maskini mashinani zisizokuwa na uwezo wa kumudu gharama kubwa ya kununua mafuta taa.

Lengo lao likiwa ni kubadilisha mfumo wa maisha kwa raia wanaokaa mashambani na mitaa ya mabanda, kwa kuwapatia ujuzi wa kujitegemea huku wakiyalinda mazingira yao.

Stovu ya kisasa inayotumia kawi safi. Picha/ Maggy Maina

NCCBO ilianzishwa kisha ikaendeshwa na Bw Tom Agosa yapata miezi minne iliyopita.

“Tangu serikali kupiga marufuku ukataji miti kwa ajili ya kuchoma makaa,tulihusisha serikali ili kuwafaidi wananchi wasije wakataabika,”akasema.

Toyokomi ilieleza Taifa Leo Dijitali kuwa walipata ujuzi huu baada ya kuzuru nchi ya Afrika Kusini, ambapo iliibuka kuwa raia katika mataifa yanayoendelea hawana mbinu mwafaka ya kuzalisha kawi salama kwa matumizi,

“Bado watu wengi Afrika wanatumia kuni,samadi kupika,hali hii husababisha ajali mbaya za moto na watoto huishia kupata maradhi ya pumu pindi wanapopumua hewa ambayo si safi,”alisema.

Stovu yenyewe ina sehemu mbili ambapo hata mafuta yakimwagika hawawezi kusambaa na kusababisha moto.

Pia chuma yake ni ngumu kiasi kwamba inaweza kustahimili hali mbaya ya anga na wala haiwezi kupata kutu.

Bw Agosa alieleza kuwa serikali inajaribu kushawishi kampuni ya Toyotomi iingie humu nchini ili kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana.

Alisema stovu hizi ni za kisasa na hutumia kiwango kidogo sana cha mafuta ambapo lita mbili tu zinatosha kumchukua mtumiaji hadi masaa 20.

“Ni salama kwa afya ya wananchi ikilinganishwa na aina nyinginezo zinazopatikana sokoni,”alisema.

Mwezi huu dunia ilipoadhimisha siku ya mazingira ulimwenguni, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alinukuliwa akisema matumizi ya kawi chafu yamechangia maradhi ya kupumua na ukuaji mbaya wa watoto.