Habari Mseto

Suala la umoja wa jamii ya Waluhya lashamiri mkutano wa BBI Kakamega

January 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HAJA ya kuwepo kwa umoja wa jamii ya Waluhya ilishamiri Jumamosi katika mkutano wa uhamasisho kuhusu yaliyomo kwenye ripoti ya maridhiano (BBI) mjini Kakamega.

Tofauti na ilivyodhaniwa kwamba kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula wangeususia, wawili hao walifika katika uwanja wa Bukhungu.

Walikariri kujitolea kwao kuungana na wenzao kuipigia debe ripoti ya BBI kwa ushirikiano na wenzao kuhimiza utekelezaji wa vipengele vya kufaidi wakazi wa eneo hilo.

Na viongozi kutoka maeneo mengine pia waliwahimiza viongozi hao wa Waluhya wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Cotu) kuungana ili waweze kufaidi kutokana na yaliyomo katika ripoti ya BBI.

“Huu mchakato wa BBI ndio njia ya kipekee itakayohakikisha kuwa jamii ya ‘Omulembe’ inaingia katika serikali ijayo. Kwa hivyo, nawaomba viongozi wote wa jamii ya Waluhya muungane chini ya BBI kwa kuongea kwa sauti moja,” akasema Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat.

Naye Bw Atwoli alitoa changamoto kwa Mbw Mudavadi na Wetang’ula kuvunjilia vyama vyao ili waunde chama kimoja kama thibitisho ya kwamba wamejitolea kuunga kwa masilahi ya jamii ya Waluhya.

“Ningependa kusema hapa kwamba wewe Mudavadi na Wetang’ula mwawadanganya wananchi hawa kwamba mmeungana. Ikiwa ni kweli basi wewe Mudavadi vunja ANC na wewe Wetang’ula uvunje Ford-Kenya ili muunde chama kimoja cha kuunganisha sisi sote kama Waluhya,” akasema Bw Atwoli.

Akaongeza: “Mudavadi na Wetang’ula ni watoto wangu. Ndio maana niliposikia kwamba hawatafika hapa niliwapigia simu nikiwahimiza kubadili nia na nafurahi kwamba wameitikia himizo lango.”

Naye Waziri Eugene Wamalwa alielezea furaha yake kwamba mkutano huo wa BBI ilifaulu kuwaleta pamoja viongozi wote wa jamii ya Waluhya.

“Sasa nina imani kwamba ndoto yetu ya kuungana kama jamii kwa manufaa ya watu wetu itatimia. Nimefurahi zaidi kuwaona ndugu zangu Mudavadi na Wetang’ula hapa leo (Jumamosi), ishara kwamba sote tu pamoja,” akasema Waziri huyo wa Ugatuzi.

Mkutano huo uliongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga na ukahudhuriwa na viongozi kutoka pembe zote za nchini. Wote walikariri kuunga mkono mchakato wa BBI.