Sukari ya nje nchini yapungua pakubwa
Na BERNARDINE MUTANU
Viwango vya sukari iliyoagizwa vimepungua kwa asilimia 72 tangu mwaka 2017
Ripoti hii ni kwa mujibu wa Afisi inayosimamia sukari nchini ambayo ilionyesha kuwa kiwango cha sukari kilichoagizwa nchini kilipungua hadi tani 9,907 katika kipindi cha uchunguzi kutoka tani 35, 170 katika kipindi hicho mwaka jana.
“Kiwango cha jumla cha sukari iliyoagizwa Februari 2018 kilikuwa ni 9,907 ikilinganishwa na tani 35,170 zilizoagizwa katika kipindi hicho mwaka jana, upungufu wa asilimia 72,” ilisema ripoti hiyo.
Afisi hiyo wiki jana ilisema ilikuwa ikilenga kupunguza viwango vya sukari inayoagizwa kutoka soko la nje hadi tani 7,000 kwa mwezi kutoka tani 29,000 zilizokuwa zikiagizwa kutoka awali.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kulinda kampuni za kutengeneza sukari nchini.
Kenya imekubaliwa kuagiza tani 350,000 za sukari kila mwaka kutoka kwa Soko la Jumla la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa).
Kenya iliagiza tani kufikia 900,000 za sukari kati ya Mei na Desemba mwaka jana kutokana na hatua ya serikali kuondolea waagizaji ushuru kununua bidhaa hiyo nje ya Comesa.