Habari Mseto

Taharuki huku mauaji yakirejea Kapedo

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na FLORAH KOECH

HALI ya taharuki imetanda eneo la Kapedo kwenye mpaka wa Kaunti za Baringo na Turkana kufuatia kuuawa kwa watu wawili Jumapili.

Mashambulizi hayo yamezua hofu ya kuzuka tena kwa uhasama kati ya jamii zinazopigana za Wapokot na Waturkana zinazoishi eneo hilo.

Shughuli za usafiri katika barabara ya kutoka Kapedo kuelekea Chemolingot na kutoka Kapedo kuelekea Lomelo zimekwama wakazi wakihofia kushambuliwa na wahalifu ambao inaaminika wamejificha vichakani.

Mkazi mmoja, Leng’it Long’uria, alisema wakazi walio Kapedo wamekuwa wakipata mazao ya chakula kutoka Marigat lakini hawawezi kutumia barabara ya Kapedo-Chemolingot kwa wakati huu wakiogopa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

“Tunahofia kwamba wakazi watakufa kwa njaa hapa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kutatua suala hili. Kwa kawaida huwa tunapata mazao ya chakula kutoka Marigat lakini barabara hii sasa ni hatari na wakazi wanahofia majangili watawashambulia wakiwa njiani.

Hatuwezi kufika Lokori kwa sababu tunaamini wahalifu wamejificha kwenye barabara ya kuelekea Lomelo,” alisema Long’uria.

Maduka katika soko la Kapedo yamefungwa huku wakazi wakibaki nyumbani wakihofia kushambuliwa na jamii za Wapokot na Waturkana.

Aliiomba serikali kurejesha utulivu katika eneo hilo akisema mashambulizi ya majuzi yataathiri wanafunzi wanaofanya mitihani ya kitaifa ikiwa hatua hazitachukuliwa kuimarisha usalama.

Shambulizi la Jumapili lilifanyika baada ya watu wawili kuuawa na wengine wawili kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na watu walioshukiwa kuwa majangili eneo la Kapedo.

Waliouawa walitoka eneo la Kapau, Kaunti Ndogo ya Tiaty na inashukiwa waliuawa na wahalifu kutoka Kaunti ya Turkana.

Marehemu walitambuliwa kama Ruto Lomerisiya, 21 na Kanyoria Domokamar aliyekuwa na umri wa miaka 24. Wote walikufa baada ya kupigwa risasi kichwani.

Kulingana na chifu wa lokesheni ya Kapau, Sadaam Kalale, wanaume hao kutoka Pokot walikuwa wakipeleka mifugo wao sokoni Ameyan, waliposhambuliwa. Alisema kulikuwa na ufyatulianaji mkali wa risasi kabla ya wanajeshi walio katika kambi ya Chesitet kufika.

“Bado hatujajua nia ya wavamizi kwa sababu waliwaua wanaume hao na kutoroka bila kuiba chochote,” alisema chifu huyo.

Kamishna wa Kaunti ya Baringo, Henry Wafula amelaani kisa hicho na kuhimiza jamii kutolipiza kisasi.