Habari Mseto

Taharuki uvamizi wa majangili ukirejea

June 8th, 2024 1 min read

NA OSCAR KAKAI

VISA vya ujangili na wizi wa mifugo vimerejea kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet baada ya miezi mitano ya utulivu.

Hali ya taharuki inaendelea kutanda katika kijiji cha Kamelei kilichoko kaunti ndogo ya Pokot Kusini, kaunti ya Pokot Magharibi baada ya washukiwa wa ujangili kutoka kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet kuvamia kijiji hicho na kuiba mifugo idadi isiyojulikana mnamo Alhamisi asubuhi.

Mashambulio hayo mapya yamewakera wakazi ambao waliamua kufanya maandamano.

Walilamikia ongezeko la mashambulizi, wizi wa mifugo pamoja na kile walidai ni uzembe wa maafisa wa usalama wanaohudumu katika eneo hilo.

Waandamanaji walifunga barabara ya Kapsangar-Kamelei huku shughuli za kawaida zikisitishwa kwa muda.

Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya msichana wa umri wa miaka saba kupigwa risasi na kuuawa na majangili katika eneo la Kamologon.

Soma Pia: Majangili waua msichana na kuiba mifugo Kamologon

Naibu Kamishina wa kaunti ndogo ya Pokot Kusini David Bowen alisema serikali ilifika kwa wakati kusaka majangili na mifugo walioibiwa.

Alisema kuwa askari wa akiba (NPR) 15 watatumwa eneo hilo.