'Tangatanga' sasa wamtetea Ndindi Nyoro
Na NDUNGU GACHANE
VIONGOZI wa Chama cha Jubilee wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto chini ya kikundi kilicho maarufu kama ‘Tanga Tanga’, wamemjibu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumsuta mmoja wao hadharani.
Alhamisi iliyopita, Rais Kenyatta alimkashifu vikali Mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro na kudai kazi yake ni kutangatanga sehemu tofauti za nchi na kuhudhuria mikutano chungu nzima badala ya kufanyia kazi wananchi katika eneobunge lake.
Matamshi ya Rais yalitokea wakati wa mazishi ya mfanyabiashara mashuhuri Thayu Kamau baada ya mbunge huyo kumwomba Rais Kenyatta kutoa mchango wa angalau Sh5 milioni ili kuboresha Shule ya Upili ya Gitui.
Rais alimpuuzilia mbali kwa hasira na kumtaka kwanza aeleze jinsi alivyotumia Sh100 milioni za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji wa Maeneobunge, huku umati ukishangilia.
Lakini kikundi cha Tanga Tanga jana kilijibu matamshi ya Rais na kusema wana imani kubwa kwa uongozi wa mbunge huyo anayetumikia kipindi chake cha kwanza.
Wakiongozwa na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, walimsifu Bw Nyoro na kudai amefanya kazi shwari akiwa Mbunge wa Kiharu.
Kulingana na Bw Kuria, mbunge huyo ana haki za kutaka maendeleo katika eneobunge lake na hakuwa anaomba msaada bali haki ya wakazi wa eneobunge hilo.
“Ni haki ya kila kiongozi kuitisha na wala si kuomba maendeleo katika maeneo yao kwa sababu hata watu wa Murang’a hulipa ushuru tena ushuru mkubwa mno kutoka kwa kilimo cha kahawa na chai,” akasema.
Mtazamo sawa na huu ulitolewa na Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome ambaye alisema ingawa wanaunga mkono serikali, “kuna pengo la kimaendeleo na tutazidi kuitisha rasilimali ili ziongezwe ikiwemo maji na upanuzi wa barabara Murang’a.”
Akizungumza mbele ya Bw Ruto, mbunge huyo alisema Naibu Rais yuko huru kutembelea kaunti hiyo wakati wowote huku akidai kuna watu ambao hawafurahishwi na jinsi anavyopata umaarufu kwa wakazi wa Mlima Kenya.
“Tutaendelea kukuunga mkono na tunataka chama chetu kiwe imara ili kuzuia mashambulio ya mara kwa mara kutoka nje,” akasema.
Kwa upande wake, Kiranja Mkuu wa Seneti aliye pia Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika alimsifu Bw Nyoro kwa kusimamia vyema fedha za umma.
Alieleza wasiwasi wake kuhusu vita dhidi ya ufisadi na kudai vinatumiwa kisiasa.
“Ufisadi ni suala nzito katika nchi hii lakini linafaa kukabiliwa kwa njia ya haki kwa sababu inavyoonekana, ni kama kwamba kuna lengo tofauti,” akasema.
Wengine waliomtetea Bw Nyoro ni Seneta Maalumu, Bw Isaac Mwaura na Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu ambao walisema hakuna kitakachowazuia kumpigia debe Bw Ruto kwa urais wa mwaka wa 2022.