Habari Mseto

TANZIA: Dereva wa klabu ya Gor Mahia afariki

May 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

JUMUIYA ya klabu ya Gor Mahia imempoteza dereva wao wa muda wa miaka mingi Bw Patrick Osewe Agwambo aliyefariki Jumatano usiku.

Aliaga dunia njiani akisafirishwa kupokea matibabu zaidi katika eneo la Karachuonyo, Kaunti ya Homa Bay.

Alikuwa akiishi Kibra, Nairobi na amekuwa akikabiliwa na matatizo ya kiafya.

Ameugua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa benchi ya kiufundi wa Gor Jolawi Obondo, mwili wa marehemu upo kwenye mojawapo ya chumba cha kuhifadhia maiti eneo la Karachuonyo.

“Ni kwa masikitiko makuu tunatangaza kifo cha dereva wetu wa miaka mingi Patrick Osewe ‘Agwambo’. Aliaga dunia Jumatano baada ya kuugua kwa muda mrefu. Tafadhalini wekeni familia yake na jamaa kwa maombi. #Sirkal,” imesema taarifa ya klabu kwenye mitandao ya Facebook na Twitter.

Obondo alifichua kwamba alizungumza na marehemu Jumanne alipokuwa akiwalipa wachezaji na wanachama wa benchi ya kiufundi mishahara yao, na marehemu akamwambia hakuwa akijihisi vyema kiafya.

“Nilikuwa nimempokeza Samuel Onyango (mshambuliaji) fedha zake ili amfikishie kwa sababu wao ni marafiki wa karibu sana. Alikuwa mtu aliyependa kazi yake, mwenye utu na tutapeza sana huduma zake. Tunaomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake pahala pema penye wema,” akasema Obondo.

Nahodha wa Gor Kenneth Muguna aliwaongoza wachezaji wenzake kumwomboleza Osewe ambaye alipokezwa jina la msimbo ‘Agwambo’ kutokana na jinsi alivyoenzi siasa za Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye pia ni mlezi wa klabu.

“Nimesikitika sana kusikia kifo cha Patrick Osewe dereva wa basi la timu yetu. Alikuwa mtu mpole, mkarimu, mwenye nidhamu na aliyekuwa na mlahaka mzuri na wachezaji. Tutampeza sana,” akasema Muguna.

Osewe aliajiriwa na Gor mnamo 2012 na amemwacha nyuma mjane pamoja na watoto wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume.

Kifo cha Osewe kinajiri siku chache tu baada ya kile cha jagina wa K’Ogalo Martin Ouma ‘Ogwanjo’ Jumamosi iliyopita.

Ogwanjo ambaye alijizolea sifa kwa ustadi wake wa kuwapitisha wapinzani chenga za mauaji alizikwa mnamo Jumanne katika kijiji cha Hawinga, eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.