‘Team Wanjiku’ wapeleka kampeni Mombasa
Na WANDERI KAMAU
KUNDI la kisiasa la ‘Team Wanjiku’ linaloongozwa na Gavana wa Nairobi Mike Sonko na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuriav Jumapili litaandaa mkutano jijini Mombasa katika juhudi za kujiimarisha kisiasa nchini.
Bw Sonko anatarajiwa kuongoza mkutano katika uwanja wa uwanja wa Alidina, jijini Mombasa.
Bw Sonko ataandamana na wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Simon Mbugua (Bunge la Afrika Mashariki-EALA), wabunge wa zamani Kalembe Ndile (Kibwezi) na Reuben Ndolo (Makadara). Viongozi hao watapokewa na aliyekuwa diwani wa Jomvu, Bw Kariza Nzai.
Kundi hilo linadai kampeni zake ni za kumtetea mwananchi.
Limefanya mikutano Ruiru, Kaunti ya Kiambu na Kaunti ya Machakos tangu lilipozinduliwa.
Kundi liliwasili Mombasa jana na kufanya mikutano kadhaa na viongozi wa eneo hilo, kama matayarisho ya mkutano wa leo.
Bw Sonko alisema wamewaalika viongozi wengine kutoka Mombasa.
Kundi hilo ni la tatu kubuniwa katika Chama cha Jubilee (JP) ambacho kinakumbwa na migawanyiko ya kisiasa. Makundi mengine ni ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke.’
Bw Sonko anashikilia kuwa makundi hayo yanaendeleza siasa za 2022 bila kutilia maanani maslahi ya wananchi.
“Kuna siasa nyingi zinazoendelea kuhusu 2022, lakini tunasahau kuwa kuna mambo yanayohitaji kushughulikiwa kwanza kama bei ya juu ya unga,” akasema Bw Sonko.