Habari Mseto

Teknolojia kutumika pakubwa Mlima Kenya kukabiliana na pombe haramu

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI imezindua mbinu mpya ya kutambua ilipo pombe haramu kwa kutumia vifaa vya kiteknolojia ambavyo ni ndege zisizo na rubani, drones.

Ndege hizo zinazunguka juu hewani kwa umbali wa hadi kilomita moja mraba kutafuta maeneo halisi kunakopikwa na kutengenezwa pombe haramu.

Kamishna wa eneo la Kati Bw Wilfred Nyangwanga alisema mpango huo ukitekelezwa kikamilifu pombe haramu itaangamizwa kabisa hasa katika eneo lake.

Alisema kwa muda wa mwezi mmoja uliopita amefanya kikao na maafisa wote wakuu wa serikali pamoja na machifu wote chini ya himaya yake ili kuweka mikakati kabambe ya kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya.

“Tumefunga maskani zote za burudani; hasa baa zilizoko mita 300 kutoka kwenye shule na makazi ya watu,” alisema Bw Nyangwanga.

Alisema kwa wiki moja maskani tisa za kupikia pombe haramu tayari zimefungwa na bado zingine zitaendelea kufungwa.

“Nimetoa ilani kali kwa machifu ambao ni wazembe kuwa pombe haramu ikipatikana katika maeneo yao ni vyema wakajitayarisha kwenda nyumbani,” alisema kamishna huyo.

Aliongeza kwamba kwa mwezi mmoja uliopita watengenezaji pombe haramu wapatao 100 wametiwa nguvuni na kushtakiwa mahakamani.

Kufuatia kampeni ya kupambana na pombe haramu, tayari baa 20 zimefungwa ambapo ilibainika wengi walikuwa wakiendesha biashara hiyo bila kuwa na leseni maalum.

Mnamo Jumatatu, afisa huyo na kikosi chake walizuru maeneo ya Makwa, Mang’u, na Gatanga ili kujionea hali ilivyo mashinani.

Afisa mkuu wa kupambana na dawa za kulevya kutoka idara ya NACADA, Bw Victor Okioma aliyeandamana na kamishna huyo. alisema idara hiyo itafanya juhudi kuona ya kwamba inafanya kazi pamoja na serikali ili kuangamiza kadhia hiyo.

“Tutahakikisha tunafanikiwa kwa kazi hiyo kwa sababu tayari tumeweka mikakati ya kutosha,” alisema afisa huyo.

Alisema ya kwamba idara yake itahakikisha ajenda kuu nne za serikali zinafanikiwa ifikapo mwaka wa 2022.

“Tutafanya kazi na wanahabari ili kufanikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya na pombe haramu,” alisema Bw Okioma.

Naye mkazi mmoja wa kijiji cha Makwa eneo la Mang’u, Gatundu Kaskazini Bw Evans Kamau alisema kutokana na ushirikiano na machifu wa eneo hilo, wamefanya kazi kubwa ya kuangamiza pombe hiyo katika kijiji hicho.

“Siku hizi pombe haramu imepungua kwa kiwango kikubwa huku vijana wengi wakiingilia majukumu ya maana,” alisema Bw Kamau.

Alisema wakazi wa kijiji hicho kwa kauli moja wamekubaliana kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali ili kuangamiza pombe hiyo kabisa.