Teknolojia mpya kunasa wakwepaji ushuru
Na BERNARDINE MUTANU
Walipaji ushuru watafuatwa hata ndani ya nyumba zao katika hatua mpya ya kuwapata wakwepaji ushuru.
KRA sasa imeanza kutumia teknolojia kuwapata watu hao. Itakusanya data ya kimaumbile ya walipaji ushuru kwa kutumia mtambo na maeneo wanakoishi kwa kutumia setilaiti.
“Matumizi ya teknolojia ni muhimu sana na suala la dharura kwa KRA katika operesheni zake kutoka kwa utoaji wa huduma kwa wateja na ukwepaji kulipa ushuru. Matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kutambua mtindo wa ulipaji na upungufu wa ushuru,” alisema Rais Uhuru Kenyatta wakati wa siku ya kuadhimisha walipaji ushuru bora 2018, Nairobi Jumatano.
Mfumo tangamani ulio na uwezo mkubwa wa kusimamia ulipaji wa ushuru (NIIMS) unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Rais Uhuru Kenyatta anaitaka KRA kutumia mfumo kufuata wakwepaji ushuru kwa sababu utakuwa na habari zote za wananchi.
Hivi karibuni, serikali itaanza mchakato wa kusajili upya wananchi mwaka huu.