Habari MsetoSiasa

Tetesi Kidero atawania ugavana Homa Bay baada ya ushindi wa Awiti kufutwa

February 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero. Picha/ Maktaba

JUSTUS OCHIENG  na BARRACK ODUOR

HUENDA aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero akawania ugavana katika Kaunti ya Homa Bay.

Aidha, mkakati wa kumrai Dkt Kidero kuwania nafasi hiyo unatokana na uhasama mkali uliopo kati ya Gavana Cyprian Awiti, ambaye ushindi wake ulifutiliwa mbali na mahakama, na aliyekuwa mbunge wa Kasipul, Bw Otieno Magwanga.

Wadadisi wanasema uhasama huo umekuwa ukichangia pakubwa ukosefu wa maendeleo katika kaunti hiyo. Na kutokana na hali ilivyo, huenda ODM ikalazimika kuandaa shughuli mpya ya mchujo ili kuwavutia wawaniaji zaidi, ili kupunguza taharuki hiyo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM, Wakili Edward Sifuna alisema kwamba hawezi kusema lolote kuhusu mkakati huo kwani ni sawa na “kuzua hali ambazo hazipo.”

“Gavana Awiti alisema kuwa anawasilisha rufaa. Hivyo, suala la uchaguzi mpya lingali mbali. ODM itabaki kuwa chama kinachoheshimu demokrasia,” akasema Bw Sifuna akizungumza na ‘Taifa Leo.’

Duru katika ngome ya Bw Awiti zilisema kuwa ‘hofu’ ya ujio wa Dkt Kidero ndiyo imemfanya kufika katika Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

Bw Awiti alipoteza kiti chake wiki iliyopita baada ya Mahakama Kuu ya Homa Bay kufutilia mbali kuchaguliwa kwake.

Lakini pendekezo hilo likitolewa, Dkt Kidero amebaki kimya, licha ya juhudi za kumfikia.

Jumapili, mmoja wa waandani wake wakuu hakueleza moja kwa moja ikiwa analenga kuwania ugavana.

“Analenga kuwania nafasi kubwa zaidi ya kisiasa,” akasema.