• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 AM
Thiwasco yazidi kusambaza maji mjini Thika

Thiwasco yazidi kusambaza maji mjini Thika

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya maji ya Thiwasco Water Company Ltd, tayari inazidi kuongeza vituo maalum vya kusambaza maji kwa wananchi ili kupambana na Covid-19.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw Moses Kinya, amesema wameweka vituo 11 vya maji katika mji wa Thika, huku wananchi wakiendelea kudumisha usafi ili kukabiliana na virusi vya corona vinavyosababisha Covid-19.

“Vituo muhimu tulivyoweka maji hayo ni hospitali kuu ya Thika Level Five, kituo cha Polisi cha Thika, soko kuu la Jamhuri, Juakali, na kituo cha magari cha Makongeni,” amesema Bw Kinya.

Ametoa mwito kwa wakazi wa Thika wachukue jukumu la kujituma kwa kudumisha usafi wanapofika mjini.

“Kampuni yetu kwa ushirikiano na Kaunti ya Kiambu tumeona ni vyema kusambaza maji kwa wingi ili kufuata mwito wa serikali wa kuhimiza wananchi kunawa mikono kila mara,” akasema mkurugenzi huyo.

Amesema kwa muda wa wiki moja sasa wananchi wamebadilisha mitindo yao na kuonekana kuzingatia usafi kwa kunawa mikono kila mara wanapofika katika maeneo ya biashara na afisi tofauti.

Amezidi kueleza ya kwamba hata katika makazi ya watu wamehakikisha ya kwamba maji yanapatikana kwa wingi ili kila mmoja aweze kudumisha usafi.

Hata sekta ya matatu imefuata mwito huo huku kila msafiri akilazimika kunawa kabla ya kuabiri matatu.

Kwa muda wa wiki moja iliyopita watu wengi wanafika nyumbani mapema.

Uchunguzi uliofanywa umebainisha ya kwamba hakuna msongamano wowote wa magari ifikapo jioni kwa sababu afisi nyingi za serikali tayari zimefungwa.

Nazo biashara nyingi zinafungwa mapema kwa sababu wateja wamepungua kwa kiwango kikubwa.

“Tunaomba mambo haya yaweze kurudi kama kawaida ili tuendelee kufanya biashara zetu kama kawaida,” amesema Martin Karanja ambaye anaendesha biashara ya kuuza nguo mjini Thika.

Hata wanaofanya biashara katika baa na maskani ya burudani wanasema ya kwamba ifikapo saa mbili za usiku wateja wengi huwa wanarejea nyumbani jambo linalofanya biashara kurudi chini.

You can share this post!

COVID-19: Mbunge kudhamini wasanii wenye kazi za hamasisho

MWANAMKE MWELEDI: Mtetezi mahiri wa haki za wanawake

adminleo