Habari Mseto

TSC kuchunguza vifo vya wanafunzi

April 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WAANDISHI WETU

TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) imetoa tahadhari kufuatia ongezeko la vifo na kutoweka kwa wanafunzi katika hali isiyoeleweka huku muhula wa kwanza ukikamilika.

Hii ni kufuatia kisa ambapo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Upili ya Maseno School, Kaunti ya Kisumu, alifariki wiki iliyopita. Cyril Samuel Oyungu, 14, aliaga dunia baada ya kuugua lakini wasimamizi wa shule hiyo hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Vilevile, katika Kaunti ya Nyeri, visa viwili vya wanafunzi kutoweka katika shule tofauti za upili wiki iliyopita viliripotiwa, pamoja na visa vya wanafunzi kujiua.

Mnamo Machi 11, Kennedy Fundi, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Upili ya Kangaru, Kaunti ya Embu naye aliaga dunia akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi Womens.

Hii ilikuwa baada ya Ebbie Noelle Samuel, mwanafunzi wa shule ya upili ya St Annuarite Girls mnamo Machi 9 kulala na kutoamka. Alipatikana akipambana kupumua na alipofikishwa katika hospitali ya Naidu, Thika, ikathibitishwa alikuwa amekufa.

Mnamo Machi 3, Bethwel Agolae, mwanafunzi wa Bishop Atundo Boys – Shule ya Upili ya Kimaeti katika Kaunti ya Bungoma aliaga dunia katika hospitali ya Bungoma Magharibi.

TSC sasa imesema kuwa inachukulia visa hivyo kwa uzito, kwani vinahusu maslahi ya wanafunzi wakiwa shuleni.

“Tume inachukulia visa hivyo kwa uzito sana kwani vinahusu usalama wa wanafunzi wanapokuwa shuleni,” alisema Catherine Lenairoshi, afisa wa TSC.

Visa vya wanafunzi kutoweka, aidha vimekuwa vikiongezeka, cha hivi punde zaidi kikiwa cha mwanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya Chinga, ambaye alitoweka wiki sita zilizopita.

George Gitau Ikumi alitoweka mnamo Februari 15 baada ya kutoroka shuleni siku moja kabla ya wanafunzi kwenda likizo ya kati ya muhula.

Mamake, Hellen Gitau alifahamishwa na wasimamizi wa shule kuwa mwanao alikuwa amepotea, na hajawahi kumwona tena.

Faith Nyamai, Nicholas Komu, Reginah Kinogu na Ouma Wanzala