Tuko pamoja, asema Ruto kuhusu madai ya kumwangamiza
Na PETER MBURU
HUKU fumbo kuhusu madai kuwa mawaziri fulani wamekuwa wakikutana kupanga kumuua Naibu Rais William Ruto likizidi kukosa jibu, kiongozi huyo Alhamisi alikataa kuzungumzia suala hilo.
Dkt Ruto, ambaye alikuwa amealika wanahabari katika afisi yake mtaani Karen, Nairobi jana, alikataa kujibu maswali ya waandishi kuhusu ikiwa maisha yake yamo hatarini.
Naibu Rais alikuwa akizungumza nao kuhusu kuanzishwa kwa kampeni ya kumaliza ukeketaji nchini, wakati alipoulizwa kuhusu suala hilo.
“Tuko pamoja,” ndiyo maneno pekee alitamka kama jibu, huku akiharakisha kuondoka.
Dkt Ruto alitarajiwa kuwa angalau angetoa mwanga kuhusu suala hilo, hasa baada ya kudaiwa kuwa ndiye aliyepiga simu katika Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kulalamika kuwa kuna maafisa wa serikali ambao wamekuwa wakipanga kumuangamiza.
Wanahabari walikuwa wameamua kupiga kambi nje kumsubiri akitoka wamuulize maswali zaidi, lakini maafisa wake wa usalama wakawataka waondoke.
Seneta wa Elgeyo Marakwet na ambaye pia ni mwandani wake wa karibu Kipchumba Murkomen, Jumatano alikiri kuwa Dkt Ruto amekuwa makini kuhusu usalama wake kuliko kawaida yake.
Kimya chake kinakuja wakati maafisa wa DCI wanaripotiwa kutafuta msaada wa wapelelezi kutoka Amerika (FBI) kuchunguza uhalali wa barua ambayo ndiyo ilikuwa chanzo cha madai ya njama ya mauaji.