Habari MsetoSiasa

Tumbojoto ndani ya Jubilee baada ya Murathe kujiuzulu

January 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

BENSON MATHEKA na WANDERI KAMAU

NAIBU Mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe, Jumapili alijiuzulu wadhifa wake akisema hangeendelea kuhudumu katika kamati moja na Naibu Rais William Ruto.

Japo alisema maoni yake kumhusu Bw Ruto ni ya kibinafsi, Bw Murathe alisema hawezi kuketi katika Baraza Kuu la chama cha Jubilee na Bw Ruto na akaapa kwenda kortini kuhakikisha hatamrithi Rais Uhuru Kenyatta.

“Siwezi kuendelea kuwa naibu mwenyekiti wa chama, ikizingatiwa nitakuwa nikiketi katika baraza kuu na mtu ambaye nitaenda kortini kuzuia asigombee urais,” alisema.

Bw Murathe alisema matamshi yake hayafai kuchukuliwa kama ya Rais Kenyatta. “Ninapoongea, huwa ninaongea kama David Murathe na maoni yangu ni yangu. Ninashangaa watu wanachukulia maoni yangu kuwa ya rais,?” alisema.

Hatua yake ilijiri baada ya kushutumiwa vikali na wabunge wa Jubilee kwa mfano mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Ngunjiri Wambugu akimlaumu kwa kukiuka taratibu za chama na kanuni zinazopaswa kuzingatiwa na viongozi wakuu wa Jubilee.?“Bw Murathe anapaswa kuondoa kauli zake zote zinazohusu siasa za 2022, kwani anakiuka onyo alilotoa Rais Uhuru Kenyatta kwa wanasiasa kutojihusisha na kampeni za uchaguzi huo,” akasema Bw Wambugu.

Mbunge huyo alisema kuwa ikiwa Bw Murathe atashindwa kufanya hivyo, basi anapaswa kujiuzulu kutoka uongozi wa chama badala za kuzua migawanyiko isiyofaa. Awali kiongozi wa wengi katika seneti, Kipchumba Murkomen, alimwambia Bw Ruto asitishwe na watu wanaomwekea vizingiti katika azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Murkomen ambaye ni mwandani wa Bw Ruto alimwambia asitarajie mteremko katika azima yake ya kuwa rais akisema safari ya kuelekea ikulu huwa na vizingiti vingi na ni walio jasiri wanaofaulu.

Akiongea katika kanisa la Rivival Sanctuary mtaani Riruta, Nairobi alipoungana na wabunge kadhaa wa Jubilee wanaomuunga Bw Ruto, Murkomen alisema kama ingekuwa rahisi kuwa rais, kila mtu angekalia kiti hicho.

“Mimi nimemwambia Naibu Rais, safari ya kuwa rais sio rahisi na kama ingekuwa rahisi, kila mtu angekuwa rais,” alisema Bw Murkomen.

Akinukuu Bibilia, Bw Murkomen alifananisha masaibu ya Bw Ruto na aliyopitia Nehemiah alipokuwa akijenga ukuta wa Jerusalem.

“Waliokuwa wakimpinga Nehemiah walitumia mbinu zote lakini hawakumweza. Baadaye walimuita wazungumze lakini hakuwa na wakati wao, aliendelea kujenga ukuta,” alisema.

Katika matamshi yaliyomlenga mwenyekiti wa Jubilee David Murathe ambaye ameapa kumzuia Bw Ruto kupata tiketi ya chama cha hicho kugombea urais, Murkomen alisema wanaomdharau Naibu Rais watashangaa.

Baadhi ya maafisa wa chama cha Jubilee wakiongozwa na Bw Murathe wamesema kuwa Bw Ruto anafaa kustaafu siasa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Akizungumza alipohudhuria mazishi ya ndugu ya Katibu Mkuu wa chama hicho Raphael Tuju eneo la Rarieda, Kaunti ya Siaya mnamo Jumamosi, Bw Murathe alisema ataenda katika Mahakama Kuu kuhakikisha Bw Ruto hatakuwa rais wa Kenya.

Lakini Bw Murkomen alisema wanaotaka kuzima ndoto ya Naibu Rais ya kuwa rais wanamjenga zaidi. “Hakuna wakati ambao ilikuwa rahisi kuwa rais, ni lazima mtu astahimili na kuvuka vizingiti vingi,” alisema.