Habari MsetoSiasa

Tumesota, ODM sasa walilia ufadhili

May 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RUTH MBULA

CHAMA kikubwa zaidi cha upinzani nchini ODM, kimekiri kwamba hazina yake imesalia bila chochote na hivyo basi hakiwezi kuendesha shughuli zake wala kugharimia uchaguzi wa viongozi wake mashinani.

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed ambaye pia ni Mkurugenzi wa uchaguzi wa ODM, Jumapili alisema chama hicho hakina hela huku akiitaka Wizara ya Fedha kutoa pesa za kufadhili vyama vya kisiasa ili viweze kuendesha shughuli kama kawaida.

Bw Mohamed ambaye ni mshirika wa karibu wa Kinara wa ODM Raila Odinga akizungumza mjini Migori, alisema ukame huo wa pesa umechangiwa na ‘kiburi’ cha serikali kuendelea kukiuka katiba kwa kutotoa hela za vyama bila kutoa sababu za kuridhisha.

“Vyama vya kisiasa vina haki kupata mgao wa fedha kutoka kwa Hazina Kuu ya Fedha kwa kuwa katiba inasema hivyo. Serikali haina sababu yoyote kukosa kutoa fedha kwa vyama vinavyostahili mgao huo,” akasema Bw Mohamed.

Kulingana na sheria ya vyama vya kisiasa iliyorasimishwa mwaka 2011, vyama hivyo vina haki ya kupata asilimia 0.3 za mapato ya serikali ambazo ni Sh3 bilioni katika mwaka huu wa kifedha. Hata hivyo, hazina kuu imekuwa ikitoa tu sehemu ya pesa hizo tangu mwaka wa 2013 kwa vyama vya ODM na Jubilee ambavyo vinastahili kuzipata kulingana na idadi ya viti vilivyoshinda kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2017.

Kauli ya Bw Mohamed iliungwa mkono na Katibu wa ODM Edwin Sifuna, aliyemshutumu Waziri wa Fedha Henry Rotich kwa kukataa kufuata sheria na kuipa ODM haki yake.

Bw Sifuna alisema chama hicho kinahitaji Sh5 milioni kuandaa uchaguzi wa mashinani lakini hakiwezi kuendelea na mpango huo kutokana na ukosefu wa fedha hizo.

“Sisi tunataka fedha zetu zote kwa mkupuo kwa sababu shughuli zetu zote zimekwama kutokana na ukosefu wa pesa,” akasema Bw Sifuna akizungumza katika Kaunti ya Migori kwenye hafla ya kumkaribisha nyumbani Mbunge wa Nyatike Tom Odege wikendi iliyopita.

Chaguzi ndogo za maeneobunge ya Ugenya na Embakasi Kusini zimetajwa kama kati ya shughuli zilizofilisi hazina ya ODM pakubwa, hali ambayo sasa inatishia kulemaza kabisa mipango ya chama hicho ambacho kimekuwa chini ya himaya ya Bw Odinga tangu kibuniwe mwaka wa 2005.

Hata hivyo, hazina kuu mwezi uliopita iliashiria kwamba haina fedha za kutoa kwa ODM na Jubilee pale ilipopendekeza sheria kuhusu ufadhili wa vyama vya kisiasa ibadilishwe, kwa sababu mabilioni yanayotengewa vyama hivyo huathiri pakubwa bajeti ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Tangu mwaka wa 2015, hazina kuu imekuwa ikitoa Sh371 milioni kila mwaka badala ya zaidi ya Sh3.6 bilioni zinazofaa kutolewa kulingana na sheria.

Bw Rotich alieleza bunge mwezi uliopita kwamba kati ya mabadiliko kwenye sheria ya vyama vya kisiasa yanayofaa kukumbatiwa ni kupunguza kiasi cha fedha zinazotengewa vyama hivyo.