Habari Mseto

TUONGEE KIUME: Demu wa kuomba nauli ni hatari; muepuke

Na BENSON MATHEKA June 22nd, 2024 2 min read

KAKA, ni mademu wangapi wamewahi kula fare yako na kuingia mitini wakakuacha ukisononeka? Ikiwa ni kadhaa, makosa ni yako. Unaalika hasara kwa kutoa moyo wako kwa vipusa wasiokufaa ambao lengo lao ni kukufyoza.

Na ni wengi tu.

Vipusa wakiona mwanamume mwepesi wa kutoboka pesa, hawamwachi, wanamtumia vilivyo kujinufaisha na hawajuti.

Achana na gold digger, changamkia kipusa anayejimudu, anayeweza kujilipia nauli ya kukutembelea au kufika mnakopanga kukutana kwa miadi.

“Msichana asiyemudu  nauli ya kutembelea mtu ambaye anadai kuwa anampenda ni hasara na hatari, muambae kabla haujalia kwamba ametafuna fare,” asema mshauri wa masuala ya mahusiano ya mapenzi Samuel Femi.

Epuka mwanamke ambaye hawezi kukupatia zawadi ya siku ya kuzaliwa au valentino lakini anatarajia umzawidi ulimwengu mzima siku yake ya kuzaliwa ikifika.

Kulingana na Femi, mwanadada ambaye hawezi kukupigia simu kwa dakika 5 kabla ya kukuomba credo na kuomba data hakuwazii mazuri.

“Ninashangaa jinsi baadhi ya wanaume wanavyovumilia  wanawake wanaofikiri uhusiano ni kazi ambayo mwanadada anatakiwa kulipwa na kutunzwa? Huenda hata asikuruhusu kuramba asali huku akiendelea kukufyoza kwa kukuomba hela kila mara. Tafadhali, epuka mwanadada anayekutumia,” asema Femi.

Acha kuchumbiana na kipusa asiyekoma kukuomba pesa hata awe mrembo kiasi gani. Urembo ni bonasi, zingatia mambo mengine  muhimu kwanza. Tafuta mwanadada anayeweza  kuongeza thamani  katika maisha yako. Mwanadada anayeweza kuwekeza hisia zake kwako unavyowekeza kwake na ziwe halisi.

“Tafuta mwanadada anayeweza kukusaidia kujijenga kifedha, kimwili na kiroho. Aliye  na uwezo wa kusimamia na kuzidisha chochote ulichonacho na wala sio kutegemea unachompa na nafsi yako itakuwa na amani! Mtu ambaye hatakuwa akiketi kitako asubiri kupokea kutoka kwako,” asema Femi.

Hii haimaanishi awe tajiri. La Hasha. “Hatusemi lazima awe tajiri. Lakini awe na kitu cha kufanya hata kiwe kidogo kiasi gani, kwa sababu hata uwe na pesa kiasi gani, lazima aweze kukusaidia wakati wa shida,” aeleza Femi.

Makosa ya mabarobaro  wengi, ni kupagawishwa na umbo na sura hadi wanasahau sifa za mwanamke mzuri ni tabia na kuwa moyo safi.

“Hatusemi ni makosa mwanamume kuvutiwa na urembo wa vipusa. Kipendezacho moyo ni dawa, lakini kuna zaidi ya urembo. Mwanamke mwenye tabia nzuri na moyo safi ni tunu kwa mwanamume. Sio wale wanaosababishia wanaume mfadhaiko kwa kuwataka kutuma fare wawatembelee na kisha wanaingia mitini na kuzima simu,” asema Femi.