Tusifunike uzuri wake Moi kwa mabaya yake – Viongozi
Na WANDERI KAMAU
RAIS Mstaafu Daniel Moi alikuwa kama binadamu wa kawaida, hivyo hapaswi kulaumiwa kwa baadhi ya makosa yaliyotokea wakati wa utawala wake, wamesema viongozi mbalimbali nchini.
Wakitoa rambirambi kwa familia yake katika eneo la Kabarnet Gardens jijini Nairobi jana, viongozi hao walisema kuwa badala ya lawama, Wakenya wanapaswa kumkumbuka Moi kwa michango mingi aliyotoa ili kuboresha maisha yao.
Viongozi hao walijumuisha magavana, maseneta, wabunge, viongozi wa vyama vya wafanyakazi kati ya wengine.
Baadhi ya waliotoa kauli zao ni Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Bw Mwangi wa Iria, Seneta James Orengo (Siaya), Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU) Bw Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Bw Wilson Sossion kati ya wengine.
Akizungumza kwa niaba ya magavana, Bw Wa Iria, ambaye pia ni gavana wa Murang’a, alimsifu Mzee Moi kwa kuwa mwanzilishi wa mfumo wa ugatuzi, wakati akiwa katika chama cha KADU.
Alisema kuwa Bw Moi alikuwa mwenye maono makubwa, kwani aligundua kwamba Kenya ilihitaji mfumo huo miaka mingi iliyopita kabla ya viongozi wengine.
“Ni dhahiri kwamba Mzee Moi ndiye ‘Baba wa Ugatuzi.’ Aligundua hilo, wakati KADU ilianza kushinikiza mfumo wa majimbo kama ambao ungeifaa Kenya zaidi. Kifo chake ni pigo kubwa kwa mfumo huu,” akasema Bw Wa Iria.
Sawa na viongozi wengine, alisema kuwa ingawa kuna matatizo kadhaa yaliyoukumba utawala wake kama ufisadi, kunyamazishwa kwa wakosoaji wake na mauaji tata ya baadhi ya viongozi wa kisiasa, kuna mengi ambayo alifanya yanayowafaidi Wakenya hadi sasa.
Bw Orengo pia alitoa kauli kama hiyo, akisema kuwa sheria iliyokuwepo ilimpa Mzee Moi uwezo wa kufanya baadhi ya maovu yaliyotokea, kwani Katiba ya wakati huo ilimpa rais mamlaka kupita kiasi.
“Kijumla, Mzee Moi alikuwa kiongozi mzuri. Ingawa kuna matatizo yaliyoukumba utawala wake katika nyakati kadhaa, hayo hayapaswi kufunika mazuri aliyofanya,” akasema Bw Orengo.
Seneta huyo alikuwa miongoni mwa viongozi waliokabiliwa vikali na polisi kwa kuishinikiza serikali ya Mzee Moi kurejesha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa katika miaka ya tisini.
Mbali na hayo, alisifiwa pakubwa kwa mchango wake katika sekta ya elimu.
Bw Sossion alisema kuwa Mzee Moi atakumbukwa kwa kuwa mwanzilishi wa KNUT, kwani ndiye, aliwasilisha hoja ya kubuniwa kwa chama hicho mnamo 1957 akiwa mbunge.
Vilevile, ndiye alisajili Chama cha Kitaifa cha Walimu wa Vyuo Anuwai (KUPPET) mnamo 1998.
“Mzee Moi atakumbukwa daima kwa juhudi zake kujali maslahi ya walimu,” akasema.