Uchaguzi wa kamati za seneti waanza
Na CHARLES WASONGA
MCHAKATO wa uchaguzi wa viongozi wapya wa kamati za Seneti kuchukua nafasi ya wandani wa Naibu Rais William Ruto waliotimuliwa Mei umeanza Jumatatu.
Nafasi za maseneta hao walioondolewa kwa madai kuwa waliasi msimamo na maagizo ya Rais Uhuru Kenyatta zilijazwa na maseneta wa vyama vya upinzani, ODM na Wiper, ambavyo vinashirikiana na Jubilee.
Katika uchaguzi uliofanyika katika kamati ya Ugatuzi, Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ alipewa wadhifa wa mwenyekiti huku naibu wake akichaguliwa Seneta wa Lamu Anwar Oloitiptip.
Wadhifa ambao amekabidhiwa Bw Kajwang’ awali ulishikiliwa na Seneta wa Laikipia John Kinyua ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.
Naye Seneta wa Kitui Enock Wambua amechaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo.
Seneta wa Embu Njeru Ndwiga ataendelea kuhudumu kama mwenyekiti wa kamati hiyo.
Lakini Kamati ya Seneti kuhusu Elimu imepata mwenyekiti mpya baada ya Seneta Maalum Dkt Alice Milgo kuchaguliwa bila kupingwa. Nao wadhifa wa Naibu mwenyekiti umemwendea Seneta maalum wa ODM Dkt Agnes Zani.
Na katika uchaguzi uliofanyika katika kamati ya Seneti kuhusu Kawi, Seneta wa Nyeri Ephraim Maina amechaguliwa bila kupingwa kuendelea kuhudumu kama mwenyekiti naye Seneta Maalum Victor Prengei akachaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti.
Sura ya Kenya
Kiranja wa wengi Irungu Kang’ata amesema ujumuishwaji wa maseneta wa upinzani katika uongozi wa kamati za seneti umeidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta.
“Nimepokea maagizo kutoka kwa Rais kwamba uongozi wa kamati za seneti uakisi sura ya Kenya. Viongozi wapya ni maseneta wenye weledi mkubwa ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya Kenya. Hali hii itafanikisha majukumu ya Seneti kwani maseneta wenye ujuzi na taaluma watapata nafasi ya kuongoza kamati hizo,” Bw Kang’ata akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.