Habari Mseto

Uchambuzi wa Kitabu 'Mbio Kuhimiza Umoja wa Afrika'

October 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Waandishi: Ursula Wafula na Brian Wambi

Mchapishaji: African Storybooks Initiative

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Novela ya Watoto

Mtafsiri: Ursula Wafula

Jina la Utungo: Mbio Kuhimiza Umoja wa Afrika

HAMJAMBO watoto? Je, mnafahamu kuhusu umuhimu wa umoja katika jamii? Je, kuna baadhi ya athari za ukosefu wa umoja unazozijua?Umoja na utangamano ni nguzo kuu katika maisha ya kila jamii.

Ni vigumu kwa jamii ama nchi yoyote kuwepo bila mshikamano miongoni mwa wanajamii wake.Huu ndio ujumbe mkuu ulio kwenye hadithi ‘Mbio Kuhimiza Umoja wa Afrika.’

Hadithi hii inawahusisha vijana wawili; Kadogo na Juma. Wawili hao ni marafiki wa karibu na walipenda kukimbia karibu kila siku.Siku moja, Juma alimwambia Kadogo wakimbie ili kuhimiza umoja katika bara la Afrika.Bila pingamizi, Kadogo anakubali wazo hilo, kwani baada ya kuliwazia, aliona likiwa la maana sana.

Wawili hao waliamua kubeba kurunzi ya umoja kwenye mbio zao. Kurunzi hiyo ilikuwa kama ishara kuonyesha kwamba lengo lao kuu lilikuwa kuhimiza amani na umoja miongoni mwa jamii mbalimbali barani Afrika.

Walianzia mbio hizo katika upande wa kusini, jijini Cape Town, Afrika Kusini.Kutoka Afrika Kusini, walielekea kusini mwa bara kupitia eneo la magharibi. Walipitia nchi za Angola, Namimbia, Kongo na Cameroon.

Kwa kuwa walikuwa wameenda safari ndefu, waliamua kupumzika jijini Abuja, Nigeria.Wakimbiaji kutoka Afrika Magharibi waliamua kujiunga nao nchini Nigeria.

Waliendelea pamoja kwa kuufuata Mto Niger.Walipofika Mali, walikumbwa na upepo mkali. Juma aliwashinda wote kwa nguvu. Alijitwika jukumu na kuwaongoza wote salama.

Walipofika pwani ya Guinea, jijini Conackry, waliamua kwenda kuogelea baharini kwani walikuwa wamejaa vumbi.Baadaye, waliamua kuendelea na mbio zao kuelekea Morocco kupitia Senegal na Mauritania.

Jijini Casablanca, wakimbiaji hao waliungana na vijana wenzao na kucheza ufukoni mwa bahari.Baada ya hapo, waliamua kwenda Afrika Kaskazini.Walikimbia kupitia Algeria na Libya lakini wakapumzika nchini Misri ili kuzitazama piramidi.

Walipomaliza kuzitazama piramidi, waligeuka kusini na kuufuata Mto Nile ili kuelekea nchini Uganda.Walipita kwenye jangwa na mbuga za kitaifa.

Vijana zaidi walijiunga nao jijini Kampala, Uganda.Kutoka Kampala, vijana hao waliamua kuelekea Pwani ya Kenya.Walipofika jijini Mombasa, waliketi ufukoni wakala wali wa nazi kwa samaki.

Juma alisema waipeleke Kurunzi ya Umoja katika Mlima Kilimanjaro, nchini Tanzania. Hata hivyo, Juma alikuwa mwenye uchovu mwingi. Alianguka ijapokuwa wakimbiaji wenzake walimsaidia kuamka na kuendelea na safari.Licha ya masaibu hayo, walifanikiwa kwenda Mlima Kil

imanjaro na kuwasha Kurunzi ya Umoja. Walimalizia mbio zao nchini Zimbabwe, ambako walipokelewa kama mashujaa.Bila shaka, hadithi hii inaonyesha kwamba vijana wanaweza kutoa mchango muhimu sana katika kuhamasisha umoja na mshimamano ufaao katika jamii.

Hilo linadhihirishwa na urafiki unaoonekana miongoni mwa vijana wote wanaoungana na Juma na Kadogo. Hivyo, watoto pia wanapaswa kufahamu kuwa si jukumu la viongozi pekee kueneza umoja miongoni mwa wananchi, bali hata wao wanaweza kutoa mchango muhimu katika ustawi wa jamii.

Soma hadithi hii au itazame katika runinga yako ya NTV kila Jumatatu kuanzia saa moja na dakika 50 usiku.

[email protected]