Uchawi: Hofu vijana wakiua wazee kama njia ya kujipatia riziki
MASHIRIKA ya kijamii kaunti ya Kilifi, yametoa wito kwa juhudi za pamoja za kumaliza mauaji ya wazee kwa kushukiwa kuwa wachawi.
Mashirika hayo yanasikitika kuwa vijana katika kaunti hiyo wanaendelea kuwaua wazee na baadhi yao wamegeuza uhalifu huo kuwa ajira huku wakikodishwa kutekeleza mauaji kwa niaba ya watu wa familia za waathiriwa.
Wawakilishi wa mashirika yanayojumuisha Malindi District Cultural Association, the Malindi Gender-Based Violence (GBV) Network na Haki Yetu pia wameshinikiza kubadilishwa kwa sheria ya kuthibiti uchawi ili kujumuisha masuala ibuka.
Wakizungumza wakiwa kituo cha kitamaduni cha Mekatilili wa Menza kilichoko wadi yao Sabaki, Magarini, wakati wa ziara ya Kamati ya Watumiaji wa Korti viongozi wa mashirika hayo walisema mauaji ya wazee bado yanaendelea katika kaunti hiyo.
Kamati iliyoongozwa na Hakimu Mkuu wa Malindi Elizabeth Usui ilitembelea kituo hicho kutoa msaada wa chakula na bidhaa nyingine kwa wazee wanaohifadhiwa humo baada ya kutoroka boma zao kufuatia vitisho kutoka kwa watu wa familia zao na majirani wakishukiwa kuwa wachawi.
Katibu Mkuu wa MADCA, Bw Joseph Karisa Mwarandu alilalamika kuwa ukatili huo unaendelea kwa sababu haulaaniwi vya kutosha na viongozi wa kisiasa, kidini na maafisa wa utawala.
Alisema kwamba ni mashirika ya kijamii na kitamaduni ambayo yameachiwa vita dhidi ya dhuluma na ukatili unaotendewa wazee.
“Tatizo hili linaendelea kuzidi kwa kuwa hatusikii likilaaniwa na kila mtu. Hatusikii sauti za viongozi wa kisiasa, serikali na kidini na ndio sababu imekuwa vigumu kupigana na uhalifu huu,” alilalamika.
“Hili sio tatizo la kitamaduni. Ni suala la usalama kwa sababu kwa maoni yangu, vijana wengi wa kiume wamefanya mauaji ya wazee kuwa biashara,”alisema Mwarandu.
“Inasikitisha kwamba wauaji wanaongezeka kila siku ambao kwa sasa wanakodishwa, kwa sababu wamechukulia uhalifu huu kama shughuli ya kuwapa mapato,” alisema Bw Mwarandu ambaye ni wakili anayehudumu Malindi.
Maoni yake yaliungwa na wenzake wa Haki Yetu, Warda Zighe na Helder Lameck wa Malindi GBV Network, ambao walitaka Sheria ya Kuthibiti Uchawi ifanyiwe mabadiliko.