Uchina yajitetea tena kuhusu madai ya kutwaa bandari ya Mombasa
Na BERNARDINE MUTANU
UCHINA imekana tena madai kuwa imesababisha baadhi ya mataifa kuwa na deni kwa lengo la kutwaa mali yake.
Akiongea wakati wa maankuli ya mchana ya wahariri Nairobi, balozi wa China Kenya Wu Peng alisema makubaliano ya mikopo kati ya Kenya na China yanaambatana na viwango vya kimataifa kuhusu ukopeshaji na yanalenga maendeleo.
“Hakuna mali yoyote ya Kenya iliyouzwa kulipia mkopo wa reli ya kisasa (SGR). Hakuna mali yoyote ya Kenya itakayotwaliwa au kudhibitiwa na China, hata serikali itakaposhindwa na kulipa,” alisema Peng.
Balozi huyo wa China aliongeza kuwa kampuni za China na benki, na mashirika mengine ya taifa hilo huchunguza uwezo wa taifa wa mikopo kabla ya kutoa ufadhili wowote.
Kumekuwa na tetesi kuwa Kenya imetoa Bandari ya Mombasa kugharamia mkopo wa Exim Bank ya China, uliotumiwa kujenga SGR.
Hata hivyo, Kenya haijaweka wazi makubaliano kati yake na China kuhusiana na ufadhili wa SGR, kinyume na alivyoahidi Rais Uhuru Kenyatta mnamo Desemba wakati wa mkutano na wanahabari.
Peng alishutumu shirika la utafiti la Marekani, pamoja na taasisi za mafunzo kwa kufanya utafiti unaolenga kuharibia China jina kuhusu mikopo inayotoa kwa mataifa yanayoendelea.
“Ukweli ni kwamba hakuna taifa ambalo limenaswa katika mgogoro wa deni kwa sababu ya kushirikiana na China. Ikiwa haukubaliani na hayo, nipe mfano,” alisema.