Habari Mseto

Uchungu, lalama baada ya mtoto kufa ndani ya mtaro katika shamba la Rais Ruto, Taita Taveta

Na LUCY MKANYIKA October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Mata, Kaunti ya Taita Taveta, wamelalamika kuhusu mtaro wa mkondo wa maji uliochimbwa kwa minajili ya kusambaza maji kwa shamba kubwa la Kisima ambalo linahusishwa na Rais William Ruto, baada ya mtoto kufa maji Alhamisi iliyopita.

Mtaro huo unaopita kati ya vijiji vya Mata Chini, Ngaa, Grogan na Lesuyai, ulikuwa umesababisha kifo cha mtoto mwingine mwaka mmoja uliopita, ambapo mvulana mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu alizama.

Bw Isack Kioko ambaye alifiwa na mwanawe wiki iliyopita, alielezea alivyotamaushwa na usimamizi wa shamba hilo, akisema hakuna mtu yeyote kutoka kwa shamba hilo ambaye ameenda kwa familia hiyo kutoa pole kwa kifo cha mtoto wao.

“Hii inaonyesha hawajali. Alikuwa mtoto wangu wa pekee, naumia sana kwani kifo chake kingeweza kuzuiwa,” alisema.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Taveta Bw Nicholas Chelulot, alithibitisha kwamba ripoti hiyo ilitolewa Alhamisi katika kituo cha polisi cha Taveta.

Alisema mwanafunzi huyo wa Shule ya Msingi ya Grogan alikuwa akiandamana na mamake kuchota maji kabla ya kuteleza kwenye mtaro huo kwa bahati mbaya.

“Aliokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Taveta lakini alitangazwa kufariki alipofika,” akasema.

Bi Mercy Nzuki, ambaye mtoto wake alizama kwenye mtaro huo mwaka uliopita, alisema baadhi ya wakazi pia hujeruhiwa wanapotumbukia katika mtaro huo.

“Julai mwaka uliopita, nilimwacha mtoto wangu na watoto wengine na kwenda shambani. Niliporudi niliambiwa mtoto wangu amekufa maji,” alisimulia.

Bi Nzuki alieleza kuwa hivi majuzi aliteleza kwenye mtaro huo alipokuwa akichota maji lakini akaokolewa na wanawake wenzake waliokuwa pamoja naye.

Usimamizi wa shamba hilo ulithibitisha kuwa, wakazi walipiga ripoti kuhusu kifo cha mtoto huyo Alhamisi iliyopita.

Meneja wa shamba hilo, Bw Milton Baya, alisema wakazi wamekuwa wakipinga pendekezo la kuweka uzio wa mtaro huo wakisema wanahitaji kutumia maji yanayopita hapo.

“Wanakijiji huwa wanasema wanategemea maji ya mtaro huo kwa matumizi ya nyumbani, ndio wamekuwa wakituzuia kuuzungushia uzio. Lakini sasa itabidi tuweke uzio,” akasema Bw Baya.

Alieleza kuwa, wasimamizi wa shamba hilo watatembelea kijiji hicho leo (Jumatano) kwa madhumuni ya kushauriana na wananchi ili kuanza ujenzi wa uzio huo.