Habari Mseto

Uchunguzi wa DNA waanzishwa kubaini kama mapadri wana watoto

August 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

PETER MBURU NA STELLA CHERONO

SHIRIKA moja la kimataifa la kanisa Katoliki limelipa kampuni ya kibinafsi ya kufanya upimaji wa kubaini uzazi wa kibayolojia (DNA) humu nchini, kutoa huduma hizo kwa watoto wanaoamini kuwa walizaliwa na mapadri.

Jumamosi kampuni hiyo ilianzisha kampeni ya kuwataka kina mama ambao wamepata watoto na mapadri kutafuta huduma za DNA kutoka kwao.

Visa vya vya wanawake na watoto kulaumu mapadri wa kikatoliki kuwa walizaa watoto nao kisha kuwatelekeza vimeripotiwa humu nchini, visa vingine vikifika kortini.

Kupitia barua wiki iliyopita, papa Francis alikiri kuwa kanisa la katoliki limefeli kuzuia visa vya unyanyasaji wa kimapenzi kwa mapadri dhidi ya watoto, kwa miongo sasa.

“Kwa aibu na kutubu, tunakiri kama jamii kuwa hatujakuwa ambapo tungepaswa kuwa na kuwa hatukufanya ilivyohitajika kwa wakati uliohitajika, tukitambua kiwango cha uharibifu kilichofanywa kwa maisha mengi sana,” akaandika papa.

Mkurugenzi wa huduma za DNA Kinyanjui Murigi alisema shirika hilo kwa kipindi cha siku 30 zijazo litapokea maombi yanayohusiana na mapadri.

“Ripoti zote zitakuwa kwa siri lakini baadaye tutazipokeza kwa kanisa la katoliki na Vatican, kisha wataamua wenyewe kuhusu cha kufanya,” akasema Bw Murigi.