Habari Mseto

Uhuru aagiza KEMSA ianike tenda zote mtandaoni

September 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta ameipa Wizara ya Afya siku 30 kuanika mtandaoni zabuni zote zinazotolewa na Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa na Vifaa vya Matibabu (KEMSA).

Akizungumza jana wakati alipofunga kongamano kuhusu ugonjwa wa Covid-19 ambalo lilifanywa kupitia mtandao wa video, Rais alisema hatua hiyo itawezesha wananchi kufuatilia kila hatua ya utoaji zabuni katika shirika hilo ili ijulikane kama kuna ufisadi unaotendeka.

Agizo hilo limetokea wakati Wizara ya Afya inaendelea kulaumiwa kwa madai ya ufujaji wa pesa zilizonuiwa kusaidia katika vita dhidi ya virusi vya corona.

“Ninaagiza kuwe na mtandao ambapo zabuni zote za KEMSA zitaanikwa mtandaoni ili tuone zabuni inayotolewa, gharama yake, wanaotuma maoni ya zabuni na nani anapewa zabuni. Hii itasaidia kuhakikisha wananchi wana imani kwa viongozi waliopewa jukumu la kusimamia rasilimali za umma,” akasema.

Hata hivyo, hii haitakuwa mara ya kwanza serikali kutegemea mtandao wa kidijitali kujaribu kuzima ufisadi ambao umekolea.?Serikali tayari ina mtandao wa kutangaza habari za ununuzi wa bidhaa za umma (PPIP) ambapo matangazo yote ya zabuni za idara za umma huchapishwa.?Mtandao mwingine uliolenga kuzima ufisadi ni ule wa usimamizi wa fedha za umma (IFMIS) ambao pia umeonekana kugonga mwamba.

Wiki iliyopita, Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe na Katibu wa wizara hiyo, Bi Susan Mochache walitajwa katika kikao cha kamati ya seneti inayochunguza madai ya ufisadi kuwa walishinikiza maafisa kukiuka sheria za ununuzi wa bidhaa za umma.

Licha ya wito wa viongozi na baadhi ya wananchi kumtaka Bw Kagwe kujiuzulu, amewahi kusema kwamba hatajiuzulu.

Rais Kenyatta jana alizidi kusema kuwa, mfumo huo wa kuweka zabuni zote mtandaoni utaanza katika Wizara ya Afya kisha baadaye kuelekea kwa idara zote za serikali ikiwemo katika serikali za kaunti.