Uhuru apokea leseni mpya ya kumiliki silaha
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta, Ijumaa alipokea leseni yake mpya ya kisasa ya kumiliki silaha kufuatia agizo lililotolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kwamba watu wote wanaomiliki silaha wakaguliwe upya.
Rais Kenyatta alikabidhiwa leseni yake katika ikulu ya Nairobi na mwenyekiti wa bodi ya kutoa leseni za silaha Charles Mongera Mukindia ambaye alikuwa ameandamana na wanachama wengine wa bodi hiyo.
Kulingana na agizo hilo, wanaomiliki silaha wanatarajiwa kutuma maombi upya kufikia Machi 18 mwaka huu.
“Leo nimepokea leseni yangu mpya ya kisasa ya kumiliki silaha kutoka kwa bodi ya kutoa leseni za silaha baada ya kukaguliwa na kupata nambari maalum,” alisema Rais Kenyatta kwenye anwani yake ya Twitter.
Katika mfumo mpya ambao serikali ilianzisha mwaka jana, bodi ya kutoa leseni za kumiliki silaha itahifadhi habari zote za wamiliki wa bunduki kwenye kadi mpya ya kidijitali.
Kila anayemiliki silaha anafaa kuonyesha maafisa wa serikali kadi hiyo kila wakati akitakiwa kufanya hivyo.
Kadi hiyo ina picha ya mwenye leseni miongoni mwa habari nyingine za kumtambua.
Kulingana na Bw Matiang’i sheria hii mpya inalenga kuimarisha usalama wa kitaifa kwa kuthibiti umiliki na matumizi ya silaha.