Uhuru atangaza marufuku ya chupa za plastiki nchini
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alitangaza marufuku ya matumizi ya chupa za plastiki nchini miaka miwili baada ya serikali kuzima uuzaji, uagizaji na utengenezaji mifuko ya plastiki.
Akiongea katika Kongamano la Wanawake linaloendelea nchini Canada, Rais Kenyatta hata hivyo alisema marufuku hiyo itaanza kutekeleza Juni 5, 2020.
“Afisi za Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira zinapatikana Kenya na taifa letu limekuwa likiendesha kampeni ya utunzaji wa mazingira. Miaka miwili iliyopita tulipiga marufuku matumizi, utengenezaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki.
“Leo (Jumatano) natangaza matumizi ya chupa za plastiki ambazo hutumiwa mara moja. Marufuku hii pia itatekelezwa katika maeneo yenye ulinzi kama vile Mbuga za Kitaifa, fuo za bahari, misituni na maeneo ya uhifadhi kuanzia Juni 5, mwaka ujao,” akasema.
Rais Kenyatta alitoa tangazo hilo kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Ulimwenguni iliyofanyika sambamba na kongamano hilo.
Huku akiwapongeza wanaharakati wa zamani wa uhifadhi wa mazingira, Rais alitoa wito kwa wanawake na wasichana kukumbatia kampeni hiyo kwa sababu wao ndio huathiriwa pakubwa na shughuli za uharibifu wa mazingira.
“Kampeni za uhifadhi wa mazingira ziliongozwa na mwanamke mmoja Mkenya, Prof Wangari Mathai, ambaye alipewa tuzo ya Nobel kwa juhudi hizo mnamo 2004. Heshima hii iliyokana na juhudi zake katika kutetea masuala ya uhifadhi wa mazingira na haki za wanawake,” Rais Kenyatta akasema
“Utunzaji wa mazingira huwezesha kujengwa kwa jamii yenye afya na inayoweza kuzalisha mali. Hii ndio maana wanawake na wasichana ambao ndio waathiriwa wakuu wa uharibifu wa mazingira sharti wawe mstari wa mbele katika kampeni hizi,” akaongeza.
Mnamo Februari 28, 2017, Serikali ilizima matumizi, utengenezaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki kama hatua ya kuhifadhi mazingira.
Mataifa mengine barani Afrika, yakiwemo Tanzania, Rwanda, Mauritania na Eritrea pia yamepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.