Habari Mseto

Uhuru atuma Matiang’i kuonya Rais wa Somalia

March 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na AGGREY MUTAMBO

RAIS Uhuru Kenyatta Jumapili alikubali kutuma wakuu wa usalama kukutana na Rais wa Somalia, Mohamed Farmaajo katika hatua ya kupunguza uhasama kati ya mataifa hayo mawili.

Wawakilishi wa Rais Kenyatta waliongozwa na Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i.

Wiki iliyopita, wanajeshi wa serikali ya Somalia walipigana na wale wa Jubbaland eneo la Bula Hawa karibu na Kaunti ya Mandera, na kusababisha majeraha kwa Wakenya kadhaa ambapo mmoja alifariki baadaye.

Rais Kenyatta aliwasiliana kwa simu na mwenzake wa Somalia wakakubaliana kubuni kamati ya pamoja itakayotatua changamoto zinazosababisha uhasama kati ya nchi hizo mbili, hasa kuhusu usalama mipakani.

Dkt Matiang’i alithibitisha anaongoza ujumbe wa Rais Kenyatta nchini Somalia kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter jana.

“Kufuatia visa vingi vya ukosefu wa usalama katika mpaka wa Kenya na Somalia, maafisa kadhaa wakuu serikalini pamoja nami wametumwa na Rais Kenyatta kukutana na mwenzake wa Somalia (Faramaajo) ili kutatua masuala tata,” akaeleza Dkt Matiang’i.

Kando na usalama, uhusiano wa nchi hizo mbili ulizorota kutokana na mzozo wa mpaka Bahari Hindi.

Kesi kuhusu mzozo huo iliwasilishwa na Somalia kwenye Mahakama ya Haki Kimataifa (ICJ).

Wiki mbili zilizopita, wabunge 12 kutoka Kaskazini Mashariki nusura wajikute taabani waliposafiri hadi Somalia kukutana na rais wa nchi hiyo kwenye ziara ambayo haikuidhinishwa na serikali.

Walijitetea kwamba safari yao ilikuwa ya kibinafsi na hivyo basi hawakuhitaji kutafuta ruhusa ya serikali kuu wala bunge.