Uhuru awapa mawaziri likizo
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amewapa Mawaziri, Mawaziri Wasaidizi na Makatibu wa Wizara likizo ya siku 11 ili wapumzike pamoja na familia zao.
Hatua hiyo imeibua uvumi kwamba huenda Rais akafanya mabadiliko serikalini baada ya kukamilika kwa likizo hiyo.
Wakati wa likizo hiyo inayoanza Jumatatu, Agosti 17, 2020, hadi Ijumaa, Agosti 28, 2020, kamati mbalimbali za kiufundi za mawaziri hazitafanya vikao vyovyote.
Kamati hizo zinaweza tu kufanya vikao kwa amri ya Rais au ikiwa kuna masuala ya dharura ya kitaifa.
Katika taarifa iliyoandikwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua na kutumwa kwa mawaziri, mawaziri wasaidizi, makatibu wa wizara na Mwanasheria Mkuu, mawaziri hawatafanya ziara za kukagua miradi na mipango ya serikali katika pembe zote za nchini.
“Hata hivyo, wakati wa likizo hiyo mawaziri bado watahitajika kwenda likizo, wanaweza wakahudhuria shughuli rasmi kupitia idhini ya Rais,” akaongeza Bw Kinyua.
Baada ya likizo hiyo, Kamati ya Mawaziri kuhusu Utekelezaji wa Maendeleo inayoongozwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i itakutana mnamo Septemba 1, 2020.
Naye Rais Kenyatta ameratibiwa kuongoza kikao cha baraza la mawaziri mnamo Septemba 3, 2020, kulingana na taarifa ya Kinyua.
Likizo hiyo imeibua mjadala kwamba huenda mabadiliko yakafanyika serikalini mawaziri na makatibu wa wizara watakaporejea kazini, lakini Ikulu ya Rais imekana madai kama hayo.