Uhuru Kenyatta tuliyemchagua Rais amebadilika, Tangatanga walia
Na MWANGI MUIRURI
WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta ambao wamekuwa naye katika mkondo wake wa kisiasa sasa wanasema ametekwa nyara na mirengo inayomzingira kiasi kwamba amegeuka kabisa kiasi cha kutoeleweka.
Wengi wa wandani hao ambao wanajumuika ndani ya mrengo wa Tangatanga wanateta kuwa rais angekuwa ni bidhaa, basi wangesema leo hii Uhuru wanayemjua sio yeye ambaye anajidhihirisha kwao kwa sasa, bali ni ‘Uhuru ghushi.”
Wanalia kuwa rais wao ni kama ametekwa nyara mrengo wa Kieleweke na kufungwa kwa ‘pingu’ za handisheki na kulishwa kiapo cha kusaliti wandani wake na ambapo anakizingatia kwa uaminifu mkuu.
Tetesi ni kuwa, mirengo hiyo imemgeuza rais kuwa “sio tena yule wa kawaida ambaye alikuwa akiafikika kwa urahisi, alikuwa na nia njema kwa urafiki wa kufa kuzikana na pia aliyedhamini waliomsaidia katika safari yake telezi ya kisiasa.”
Kwa sasa, anasemwa kuwa amegeuka kuwa rais asiyeafikika kwa urahisi, haonekani kujituma kudumisha na kushikilia marafiki zake, haonekani akijituma kuwaweka wandani wake pamoja bali amejitenga kando kabisa huku hali ikigeuka kuwa si hali katika kambi yake ya kisiasa.
Hali hiyo inasemwa na wandani hao kuwa kiini cha vita vya ubabe ambavyo vimeibuka ndani ya serikali ya Jubilee huku baraza la mawaziri likionekana kugawanyika kwa mirengo ya Kieleweke, tangatanga na Handisheki.
Aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo anashikilia kuwa “huyu sio yule Uhuru aliyekuwa akituahidi mema katika kampeni zake, akiwasihi vijana wamshikilie na atawakumbuka akishinda kura ya 2013 na pia ile ya 2017. Leo hii, kinyume na yule Uhuru wa ahadi tunafahamu, amegeuka wa kutofurahisha na kutia motisha hawa vijana.”
Ni kauli ambayo imetungwa kuwa wimbo na msanii Ng’ang’a wa Kabari akiteta kuwa “huyu ni Uhuru tofauti ambaye anasimamia serikali ya kutojali maisha ya wandani wake, ya kutokuwa na shukran kwa waliomshikilia kwa dhati nay a kutozingatia kutekeleza ahadi.”
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mradi wa kiusalama wa Nyumba Kumi, Joseph Kaguthi anasema kuwa hali hiyo imezua hali ya sintofahamu ndani ya serikali na hatimaye kugeuka kuwa ukosefu wa kinidhamu na heshima “ambapo hata kuna makatibu ambao wakisema wanamwakilisha rais, wanamhujumu Naibu wa rais, Dkt William Ruto.”
Mbunge wa Bahati Kimani wa Ngunjiri anasema kuwa “mimi nimeshindwa kuielewa ni dumba gani rais amepewa na mirengo mipya ambayo imeibuka maishani mwake tangu awe rais 2013.”
Anasema kuwa “Uhuru niliyemjua alikuwa mtu wa mashinani, wa kusikia kilio cha wafuasi wake na kuwapa suluhu huku akijituma kufa kupona kuthibiti kambi yake ya kisiasa isisambaratishwe na mipigo ya kutoka nje.”
Lakini leo hii, anasema, rais mara kwa mara haeleweki hata ako wapi, akifanya nini, akiwazia nini au akipanga lipi la kesho yetu kisiasa.
Mbunge wa Embakasi Kaskazini, James Gakuya anateta kuwa rais amekuwa kimya wandani wake wakihangaishwa kushoto kulia, kupanda na kushuka kupitia sera hasi za kiuchumi hasa ubomozi wa maeneo ya kibiashara na sera hasi za kusimamia biashara.
“Sikuwa namjua Uhuru wa kuzamisha watu kwa mikopo mingi, kutosema lolote vioski vikibomolewa kiholela na mali ya wafanyabiashara kunyakuliwa na kuzuiliwa na serikali,” akasema.
Kwa mujibu wa Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, hata ikiwa ni lazima rais asimame kando na asijiangazie kama aliye na ubaguzi wa kimaebneo kwa msingi wa vyama na kabila, “kuna wasiwasi kuwa kwa sasa serikali imezidisha kiwango kinachokubalika cha kukaa bali na siasa za kimirengo.”
Bw Kaguthi anasema kuwa hali ya sasa ya Rais Kenyatta inaweza ikazua changamoto nyingi sana katika siasa na uchumi wa taifa kwa kuwa ni hali ya kuyumbisha na kuporomosha miundombinu ya uthabiti wa kisiasa na uchumi.