Uhuru, Raila wakubaliana kuhusu utekelezaji wa BBI
Na JUSTUS OCHIENG na SAMWEL OWINO
RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wanapanga kubuni mkakati wa utekelezaji wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) siku chache baada ya kuzinduliwa rasmi.
Taifa Jumapili imebaini kuwa viongozi hao wawili wako karibu kukubaliana kuhusu pendekezo la kubuniwa kwa Kamati ya Wataalamu kutathmini tena ripoti hiyo kabla ya utekelezaji wake kuanza.
Duru zilieleza kuwa viongozi hao tayari wamekubaliana kuhusu majina ya wataalamu hao, wanaotarajiwa kutajwa hadharani kabla ya mwisho wa mwaka huu ama mwanzoni mwa mwezi Januari.
“Rais Kenyatta na Bw Odinga walikubaliana kuhusu orodha ya majina hayo mapema wiki hii,” zikaeleza duru.
Wawili hao pia wamekubaliana kuhusu utaratibu wa utekelezaji wa ripoti hiyo kwa kina. Imebainika kuwa wanaonekana kutopendelea ripoti kutotekelezwa na Bunge la Kitaifa pekee, bali taasisi mbalimbali za serikali.
Hayo yalibainika kwenye mkutano kati ya Bw Odinga na Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga mnamo Jumanne jijini Nairobi. Bi Waiguru ni miongoni mwa viongozi wa Mlima Kenya ambao wamekuwa wakiipigia debe.
Kuepuka ushindani mkali
Kwenye mkutano huo, Bi Waiguru pia alifichua kuwa walijadiliana kuhusu uwezekano wa kutekeleza ripoti hiyo bila ya uwepo wa kura ya maamuzi yenye ushindani mkali wa kisiasa.
Alisema hatua hiyo inalenga kuepuka siasa za mafarakano ambazo huenda zikazua migawanyiko ya kisiasa na kikabila. Wafuasi wa viongozi hao wamekuwa wakipendelea kuandaliwa kwa kura ya maamuzi huku washirika wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto wakipigia debe mfumo wa Bunge.
Lakini mnamo Ijumaa, washirika wa Dkt Ruto walisema kuwa wako tayari kuunga mkono mfumo wowote utakaotumiwa kwenye utekelezaji wake.Baada ya mkutano huo, Bw Odinga na Bi Waiguru walisema kuwa mazungumzo yao yalilenga kuendeleza umoja nchini