Ujenzi wa kiwanda cha pombe cha Sh15B Kisumu wakamilika
Na VICTOR RABALLA
KAMPUNI ya kutengeneza mvinyo ya Kenya Breweries Limited (KBL) imekamilisha ujenzi na sasa inafanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuzindua rasmi kiwanda cha pombe kilichogarimu Sh15 bilioni jijini Kisumu.
Mkurugenzi wa KBL, Bi Jane Karuku alisema kampuni imejiandaa kuanza kutengeneza pombe aina ya Senator Keg.
“Uzinduzi wa kiwanda cha pombe utafanyika mara tu baada ya kukamilisha kufanyia majaribio mashine na miundomsingi,” akasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya KBL Afrika Mashariki, Bw Andrew Cowan alipozuru kiwanda hicho mnamo Julai, alisema kuwa bia zitaanza kutengenezwa kabla ya mwaka huu kukamilika.
Alisema kwamba KBL imeanza kushirikiana na baa 5,000 zitakazonunua pombe kabla ya kutangaza tarehe ya uzinduzi.
Alisema kiwanda hicho pia kitatengeneza aina nyinginezo za pombe kama vile Tusker.
“Tunatumia mbinu mpya ya kukusanya mtama kutoka kwa wakulima haswa katika maeneo ya Kisumu na Magharibi,” akasema Bi Karuku.
Alisema asilimia 70 ya wafanyakazi katika kiwanda hicho watatoka katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Alieleza kuwa kazi zinazohitaji wataalamu zitafanywa na wafanyakazi wa KBL kutoka viwanda vyake vilivyoko katika maeneo mengine.
“Utengenezaji wa pombe unahitaji utaalamu wa hali ya juu ambao mtu anahitaji miaka mingi kujipatia tajriba,” akasema huku akiongezea kuwa tayari kiwanda hicho kimeajiri idadi kubwa ya wafanyakazi kutoka eneo la Kisumu, mbali na kutoa nafasi nyingine za ajira kama kwa wakulima.