Habari Mseto

Ujima wa kuhakikisha wafanyabiashara, vijana na wanawake Kiambu wanapokea mikopo

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu imeingia katika mkataba na benki ya KCB na Mastercard Foundation ili kuwapa wafanyabiashara nafasi ya kupata mikopo kwa njia nafuu.

Kaunti hiyo imewekeza Sh1.3 bilioni zitakazotumika kama mikopo kwa watakaofuzu kuipokea.

Mkataba huo ulitiwa saini Ijumaa kwa lengo la kuwainua wafanyabiashara baada ya kupitia masaibu ya Covid-19 kwa zaidi ya miezi sita mfululizo.

Uzinduzi huo umetajwa kama wa kufufua uchumi kuwafaa wafanyabiashara walioathirika pakubwa wakati huo.

Kulingana na Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, hii ni njia mojawapo ya kuwainua vilivyo vijana, wanawake, na vikundi vya vyama vya ushirika vilivyopitia magumu kipindi hiki cha janga la Covid-19.

“Hii ni hatua mwafaka kwa sababu watu walioathirika wataweza kujikwamua na kujiondoa kutoka kwa magumu waliyopitia. Tuna imani ya kwamba watajiinua kwa kupokea mikopo baada ya kuwapiga jeki,” alisema Dkt Nyoro.

Kitita cha kwanza Sh138 milioni zitatolewa kwa kikundi cha kwanza.

Alisema iwapo mtu atapokea mkopo atalazimika kulipa riba ya asilimia saba badala ya 13 ya hapo awali.

Wakati huo pia vijana wamehimizwa kuchukua nafasi hiyo ya kuchukua mikopo ili kujiendeleza kwa kuanzisha na kuimarisha biashara badala ya kuketi bure.

Kulingana na gavana huyo takribani Sh600 milioni zimetengwa katika benki ya KCB zikiwasubiri vijana na wanawake wakope kwa riba nafuu.

Hata hivyo, kulingana na mpangilio huo kila mmoja atakayetaka mkopo atapokea kiwango cha Sh31,000 ili kujiendeshea biashara yake mwenyewe.

Dkt Nyoro alitoa mwito kwa vijana kujitokeza kwa wingi ili kuchukua nafasi hiyo ya kuanzisha biashara ndogo mashinani.

“Sisi kama serikali hatungetaka kuona wafanyabiashara wakitaabika huku vijana wakiingilia mambo maovu. Furaha yetu ni kuona kila mmoja akijiendeleza kimaisha,” alisema Dkt Nyoro.

Wafanyabiashara wengi walioathirika kutokana na covi-19 walipongeza juhudi za serikali ya Kaunti ya Kiambu kuwajali pamoja na vijana na wanawake.

John Kimani ambaye biashara yake iliathirika alisema hatua hiyo ni mwelekeo mzuri ambao utainua maisha ya wengi katika kaunti hiyo.

“Nina imani ya kwamba wale wote walioathirika watanufaika na mikopo ambayo itatolewa,” alisema Bw Kimani.