Umaskini na ardhi kiini cha uhalifu Kiambu
Na MARY WAMBUI
PENGO kati ya matajiri na masikini, kupanda kwa gharama ya maisha, kubadilishwa kwa ardhi iliyokuwa ya kilimo kuwa ya kibiashara na mitandao ya kijamii ni miongoni mwa sababu zinazofanya vijana wengi wa Kaunti ya Kiambu kujiunga na makundi ya kigaidi.
Haya yalifichuliwa kwenye mkutano wa wadau uliofanyika Ruiru kuandaa mikakati ya kuzuia na kukabiliana na ugaidi eneo hilo.
Washiriki wakiwemo wataalamu wa usalama, maafisa kutoka Kituo cha Taifa cha Kukabiliana na Ugaidi (NCTC), wakuu wa vikosi vya usalama na taasisi mbalimbali walisema kwamba kubadilishwa kwa ardhi kwa shughuli za kibiashara kuliacha vijana wengi bila ajira ya kujipatia riziki jambo linalowafanya kugeukia uhalifu.
Licha ya vijana wengi kukosa ajira, ripoti ya hivi punde ya Shirika la Taifa la Takwimu iliorodhesha Kiambu miongoni mwa kaunti tajiri nchini kutokana na ustawi wake katika kilimo, biashara ya kujenga na kuuza nyumba na ongezeko la viwanda.
Huku hilo likifanyika, kupanda kwa gharama ya maisha na pengo kati ya matajiri na masikini kumesababisha mitaa duni kuongezeka na mtindo ambao matajiri, baadhi wanaopata mali yao kinyume cha sheria, wanawanyanyasa masikini.
Taasisi
Kaunti hiyo ndiyo makao ya vyuo vikuu kadhaa na vyuo anuai na hivyo kulengwa na magaidi huku wataalamu wa masuala ya usalama wakionya kuwa taasisi za masomo ni miongoni mwa maeneo yanayolengwa na magaidi kusajili vijana na mashambulizi nchini.
Kulingana na Shirika la Kukabiliana na Dawa za Kulevya (Nacada), idadi ya vijana wanaotekwa na uraibu huo inaongezeka katika kaunti hiyo, ishara kwamba inatumiwa kusambaza miadharati, mianya ambayo magaidi wanatafuta kuendeleza shughuli zao bila kutambuliwa.
Wataalamu wa usalama waliohudhuria mkutano huo walisema magaidi wamebuni mbinu za kuficha vitendo vyao kuepuka kugunduliwa kwa kutumia makundi ya wahalifu yaliyomo, mitandao ya wasambazaji wa dawa za kulevya na familia zenye ushawishi kusaidia shughuli za kundi la Al Shabaab.
Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Wilson Wanyaga alisema walipata funzo kutoka kwa mshukiwa mkuu wa shambulizi katika hoteli ya Dusit2, Nairobi Ali Salim Gichunge aliyekuwa akiishi kaunti hiyo.
“Tulijifunza kwamba tunaweza kuwa na gaidi katikati yetu na kwa sababu ni mtu wa kawaida pengine aliye na mke mchanga, hauwezi kumshuku kwa sababu wote hawatoki jamii zinazojulikana kutoa magaidi. Tumegutuka sasa na ndio maana tunaandaa mikakati hii,” alisema Bw Wanyaga.