• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 AM
Umma waonywa dhidi ya kulipia kazi za sensa

Umma waonywa dhidi ya kulipia kazi za sensa

Na DENNIS LUBANGA

SHIRIKA la Kitaifa Kuhusu Takwimu (KNBS) limetahadharisha umma kuwa makini kwa baadhi ya watu na vikundi vinavyojifanya kuajiri wafanyakazi wa sensa, itakayofanywa mwaka huu.

KNBS Jumamosi ilisema kuwa ni ukiukaji wa sheria kwa mtu asiyeruhusiwa ama kundi lolote kujifanya kukusanya pesa kutoka kwa watu, kwa niaba ya shirika hilo.

Shirika hilo lilisema kuwa makundi hayo yamekuwa yakifanyia kazi kwenye mitandao, na kuwahadaa watu kuwapa pesa.

Lilisema kuwa halijampa yeyote ama kundi lolote kukusanya pesa kwa niaba yake na kuwataka watu kupiga ripoti kwa polisi ama kituo cha karibu cha shirika hilo, kuhusu watu ama makundi yanayojifanya kuwa maajenti wa KNBS.

Shirika hilo aidha limeshauri umma kwenda katika afisi zake moja kwa moja ikiwa mtu anataka kuhudumiwa, wakati muda wa watu kutuma maombi ya kazi za sensa unakamilika Jumatatu.

Akizungumza mjini Eldoret alipofanya ziara katika afisi ya Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu, mwenyekiti wa bodi ya KNBS Peter Kiguta pamoja na Mkurugenzi Mkuu Zachary Mwangi walisema kuwa zoezi la kuajiri watakaofanya kazi hiyo ni la uwazi na kuwa watakaotoa pesa kwa wakora huenda wakazipoteza, ama kupoteza nafasi zilizopo.

“Tungependa kutahadharisha watu kuwa KNBS haiitishi malipo ili mtu kupewa kazi katika zoezi la sensa. Zoezi hilo ni wazi kabisa,” akasema Bw Kiguta.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa watakaolipa pesa zozote kwa wakora watazipoteza.

“Watu wasitumie mbinu zingine kutafuta kazi za sensa kwa kuwa wakilipa pesa zozote watazipoteza, na pia wapoteze fursa,” akasema.

Bw Mwangi alisema kuwa shirika hilo linahofia huenda kuna baadhi ya Wakenya watakaojitokeza dakika za mwisho na hivyo kuhadaiwa kulipa pesa na wakora, kwa matumaini kuwa wataajiriwa kama maafisa wa sensa.

“Mkenya yeyote anaweza kutafuta kazi hizo kwa kutuma maombi kwa chifu, naibu wa chifu ama kamati ya sensa katika Kaunti Ndogo na yeyote anayedai malipo ili kupokea maombi ya kazi hizo aripotiwe kwa polisi,” Bw Mwangi akasema.

Shirika hilo lilitangaza kuwa litaajiri maafisa 136,000 kwa zoezi hilo, wa kufanya kazi ya kufanya hesabu.

You can share this post!

UGATUZI: Hatari ya shughuli za kaunti kukwama

Maisha ya wanyama pazuri baada ya Ziwa Nakuru kusafishwa

adminleo